Ronaldo kuepuka baada ya kukumbwa na madai ya unyanyasaji wa kingono

ronaldo
ronaldo
Nyota wa soka Cristiano Ronaldo hatakabiliwa na shtaka lolote baada ya kutuhumiwa na madai ya unyanyasaji wa kingono, waendesha mashtaka wa Marekani wamesema.

Mwanadada mmoja Kathryn Mayorga alidai kuwa mchezaji huyo wa klabu ya Juventus alimbaka katika hoteli moja jijini Las Vegas mwaka 2009. Inaripotiwa kwamba Mayorga alikubaliana na nyota huyo kusuluhisha kesi hiyo kimya kimya nje ya mahakama mwaka 2010.

David de Gea anasema anataka kuwa nahodha wa Manchester United baada ya kutia saini mkataba wa muda mrefu klabuni humo. Ole Gunnar Solskjaer, meneja wa United, anamtafura nahodha mpya baada ya kumwacha Antonio Valencia kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita, na akasema kwamba Paul Pogba, Chris Smalling, Ashley Young na De Gea wote wanawania wadhfa huo.

De Gea aliyejiunga na United kutoka Atletico Madrid mwaka wa 2011, anasema yuko tayari kuchukua majukumu zaidi Old Trafford na kuiongoza timu changa ya Solskjaer.

Huko Uhispania, Barcelona wako tayari kufanya mazungumzo na Lionel Messi mwenye umri wa miaka 32, kurefusha mkataba wa nyota huyo raia wa Argentina kwa miaka minne zaidi.

Kwingineko Tottenham wanajiandaa kutumia tena kitita kikubwa cha fedha wiki hii, kukamilisha usajili wa kiungo wa kati wa Real Betis na Argentina Giovani lo Celso mwenye umri wa miaka 23, pamoja na mlinzi wa Fulham na Uingereza, Ryan Sessegnon mwenye umri wa miaka 19.

Klabu ya ligi ya Uchina Beijing Guoan wamepania kumsajili winga wa Real Madrid Gareth Bale. Klabu hiyo, ina mpango wa kumfanya winga huyo mwenye miaka 30 kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika ligi ya Uchina.

Manchester United, ambao awali walikuwa wakimnyemelea Bale wamejitoa katika mbio za kumsajili mchezaji huyo. Wakati huo huo United hatimaye imekubali masharti ya kumsajili beki wa Leicester na Uingereza Harry Maguire. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 atawasili Old Trafford kwa kitita cha pauni milioni 80.