Ruto anyimwa ruhusa na Ikulu kusafiri Amerika na Canada

RAIS KENYATTA NA NAIBU RAIS WILLIAM RUTO
RAIS KENYATTA NA NAIBU RAIS WILLIAM RUTO
Ikulu ya rais huenda imemzuia Naibu Rais William Ruto kusafiri nchini Amerika na Canada, hatua ambayo huenda ikaibua joto la kisiasa na mvutano katika chama tawala cha Jubilee.

Kufutiliwa mbali kwa ziara hizo kunasemekana kuleta hali ya kutoelewana katika wizara ya mashauri ya nchi za kigeni na kupelekea mmoja wa wanadiplomasia wakuu katika wizara hiyo kupewa likizo ya lazima.

Ruto alikuwa amepangiwa kuondoka nchini Kenya siku ya Jumatatu.

Gazeti la The Star limebaini kwamba Ruto alikuwa afanye ziara katika nchi mbili akilenga kuboresha hadhi yake na kutafuta uungwaji mkono katika nchi hizo mbili. Hatua hii ingepiga jeki azma yake kuania urais mwaka 2022 mbali na kuimarisha hadhi yake kimataifa.

Naibu rais pia alinuia kukutana na wakenya wanaoishi ughaibuni, ambao ni nguzo muhimu katika maamuzi ya kisiasa humu nchini. Wengi wao watapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 2022.

Ziara hiyo ilikuwa imepangwa na maafisa kutoka ofisi ya Naibu Rais na wabunge kadhaa.

Ikulu ya rais hata hivyo ilidinda kuidhinisha ziara hiyo.

Duru za kuaminika karibu na rais za sema kwamba, Rais Uhuru Kenyatta aliamini kuwa ziara hiyo ililenga kuendeleza kampeni za Ruto za mwaka 2022.

Mwito wa rais Kenyatta kwa naibu wake na wafuasi wake kusitisha kampeni za mapema umepuuzwa huku Ruto akiendeleza kampeni zake kote nchini akitafuta uungwaji mkono.

Jana, katibu wa mawasiliano wa Naibu Rais David Mugonyi alithibisha kuwa Ruto alikuwa amepangiwa kusafiri ng’ambo.

Hata hivyo alishikilia kwamba ziara hiyo ilifutiliwa mbali kutokana na changamoto za mrundiko wa kazi huko ziara hiyo pia ikijiri wakati mmoja na ile ya rais Kenyatta.

“Rais Kenyatta anatarajiwa kusafiri nchini Afrika Kusini kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Cyril Ramaphosa kama rais wa nchi hiyo siku ya Ijumaa. Baada ya hapo rais ataelekea mjini Vancouver, Canada, kuhudhuria kongamano la Wanawake kati ya Juni 3-6,” Mugonyi alisema.

Mwaka 2016, Uhuru Kenyatta alikuwa ziarani Zambia akihudhuria kongamano kuhusu kawi barani Afrika naye Ruto alikuwa nchini Uturuki akihudhuria mkutano kuhusu haki za binadamu.