Ruto apuuzilia mbali uvumi kuwa Uhuru atasalia mamlakani

Naibu rais William Ruto siku ya Jumatatu alipuuzilia mbali uvumi kwamba rais Uhuru Kenyatta anapanga kuongeza hatamu yake ya urais.

Alisema kwamba rais Kenyatta ni mwanademokrasia na kwamba hawezi kukubali pendelezo kama hilo.

Naibu rais alisema uvumi kama huo ulikuwa unaibua hisi mseto miongoni mwa wakenya.

“Sidhani kwamba rais Uhuru Kenyatta ameambia mtu yeyote kwamba anataka kuongeza hatamu yake. Sasa hawa watu wanatoa habari hizi wapi?" Ruto aliuliza.

Naibu rais alizungumza nyumbani kwake mtaani Karen alipokutana na viongozi kutoka jamii za Waluo na Waluhya.

Wakati huo huo Ruto alitaka pafanyike mazungumzo wa wazi na yanayojumuisha kila mtu kuhusu mabadiliko ya katiba.

Alisema kwamba viongozi waonaoshinikiza kufanyika kwa mabadiliko hayo hawafai kuwatisha na kuwashurutisha wananchi kuunga mkono azma yao.

“Tunapojadiliana kuhusu katiba, wacha tuchukuliye wakenya wote kwa usawa. Tusiweke karata chini ya meza.”

Naibu rais aliwataka wakenya kusimama wima na kukataa viongozi wanaotumia njia lza kuwahadaa na vitisho il waunge mkono ajenda zao.