Ruto hakaribishwi Magharibi - Wabunge wadai

malala
malala
Kufurushwa kwa zaidi ya watu 2,000 kutoka shamba linalozozaniwa katika kaunti ya Nandi kumeibua malumbano ya kisiasa licha ya kuwepo kwa agizo la mahakama.

Wengi wa waliofurushwa na wa kutoka jamii ya waluhya. Wanadai kununua ardhi ya ekari 28 katika kijiji cha Chepturo karibu na eneo la Kaptobongen Nandi Central na wameishi hapo kwa zaidi ya miaka 40.

Lakini familia ya marehemu Kipkosgei arap Cheptulu inadai kwamba takriban familia 57 zilivamia ardhi hiyo iliyosajiliwa kwa nambari Nandi/Kapkangani /1371-1384 miaka ya sabini. Familia ya Cheptus inadai kwamba watu hao walikuwa maskwota. Maafisa wa polisi waliongoza oparesheni ya kufurusha familia hizo Jumatano usiku.

Siku ya Alhamisi, viongozi kutoka jamii ya Luhya walimtaka naibu rais William Ruto kutokanyaga katika eneo la Magharibi kama jamaa waliofurushwa hawatakuwa wamerejea makwao.

Gavana wa Nandi Stephen Sang, hata hivyo ameonya viongozi dhidi ya kuingiza siasa katika swala hilo, akiongeza kwamba linafaa kushughulikiwa kwa uangalifu – bila kuchochea wananchi. Alisema swala hili limekuwa mahakamani tangu mwaka 1979 na kwamba agizo la mahakama liliidhinisha kufurushwa familia hizo.

Sang alisema kwamba katika hali ya kutafuta suluhu kwa jambo hilo, maafisa wa serikali wakiongozwa na waziri wa Ardhi Farida Karoney walikuwa wamehudhuria mkutano shambani humo na kuafikiana kwamba serikali iwatafutiye jamaa hao ardhi mbadala au imlipe fidia mmiliki wa ardhi hiyo.

“Nasikitika kwamba vikosi vya usalama vilitekeleza oparesheni ya kuwafurusha watu kutoka ardhi hiyo kabla ya mapendekezo yaliokuwa yametolewa,” Sang alisema.

Taarifa yake ilijiri punde tu baada ya viongozi wa magharibi mwa nchi wakiongozwa na seneta Cleophas Malala, kuhoji kimya cha vigogo wa kisiasa kutoka eneo hilo.Walitaka ardhi hiyo kurejeshewa familia zilizokuwa zikiishi humo.

“Sifichi matamshi yangu. Nataka kumwambia Naibu rais: Hukaribishwi kwetu kama watu wetu wanafurushwa kutoka Nandi,” Malala alisema katika mkao na wanahabari.

Waliokuwepo wakati wa mkutano huo ni wabunge Caleb Amisi (Saboti), Florence Mutua (Busia), George Aladwa (Makadara), Geoffrey Osotsi (mbunge maalum) na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna.