Safaricom yazindua data na muda wa maongezi bila muda wa mwisho wa matumizi

Wateja wa Safaraicom sasa wataweza kununua data ambazo hazitakuwa na muda wa mwisho wa matumizi.

Afisa mkuu mtendaji wa kapuni hiyo Michael Joseph alitoa tangazo hilo wakati wa maadhimisho ya mwaka wa 19 tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo. Alizindua mfumo huo wenye kauli mbiu ‘Simple. Transparent. Honest.’

Mteja anapotaka kununua data akitumia *544#, itamletea chaguo nne: Data bundle (bila tarehe ya mwisho ya matumizi), Calls na SMS (bila tarehe ya mwisho ya matumizi), Data za kawaida zikiwa na muda wa matumizi na pata salio (Check balance).

Chini ya msimbo au code ya *544# mteja ataweza kuchagua kiasi chochete anachotaka kununua na pia kupata asilimia 50 zaidi ya pesa za maongezi na kutuma SMS kwa mitandao yoyote nchini.

Safaricom pia imesema kwamba itahududumia zaidi ya wateja wake milioni 33 chini ya muda wa dakika tano katika maduka yake yote zaidi ya 50 nchini na kila wanapopiga simu kwa kituo cha kuwahudumia wateja.

“Kampuni hiyo itaboresha maduka yake yote kote nchini ili kutoa huduma bora kwa kila mteja,” Joseph aliongeza.

Kuanzia Novemba Mosi mwaka huu, wateja wapya wanaojiunga na Safaricom watapokea kadi za simu bila malipo katika maduka yote ya Safaricom kote nchini. Mteja hata hivyo atahitajika kuweka kadi ya maongezi ya shilingi 50 kabla ya kuanza kuitumia.

Kupitia msimbo au code ya *100#, wateja wanaweza kudhibiti huduma zote ambazo wamesajiliwa, kusitisha jumbe za biashara na kudhibiti matumizi ya data. Kulingana na Afisa mkuu mtendaji, wateja hawafai kuperuzi mitandao bila data.

"Tazama matumizi ya data zako, pata dondoo za kudhibiti data na upate namba yako ya PUK," alisema.

Mpangilio huu mpya vile vile unampa mteja uhuru wa kununua kadi za maongezi na data kwa kiasi chochote kuanzia shilingi moja. Wateja wataona ni data ngapi, dakika ngapi na ni SMS ngapi mtu atapa kabla ya kukamilisha shughuli ya kuongeza kadi ya maongezi.

Kampuni hiyo pia imeongeza kiasi cha data kwa asilimia 45 kwa watumizi wa chini wa kati ya shilingi 1 – 20. Mteja anaye nunua data ya thamani ya shilingi 5 atapokea MB 10 ambazo hazitakuwa na muda wa mwisho wa matumizi kutoka MB 7 ambazo zingetumika tu kwa saa 24.

Hatua hii inajiri wakati wakili Adrian Kamotho ameishtaki kampuni hiyo kwa kuwapokonya wateja data ambazo hawajatumia.