Sakaja awashambulia Murkomen na Mutula Junior, kwa kutetea Sonko.

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja amekashifu maseneta wenzake wanaomwakilisha kama mawakili gavana Mike Sonko katika kesi ya ufisadi inayomkabili.

Kwenye mahojiano katika kituo cha Radio KISS FM siku ya Jumanne, Sakaja alisema maseneta wanajukumu la kuchunguza vile ugatuzi unaendeshwa.

Alisema hatua ya maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Mutula Kilonzo Junior (Makueni) ilionyesha kwamba wanaunga mkono ufujaji wa pesa za kaunti.

Murkomen na Mutula ni miongoni mwa mawakili wanaomwakilisha Sonko katika kesi ya ufisadi inayomkabili ya ufujaji wa shilingi milioni 357.

Sakaja alihoji vile Mutula na Murkomen watatoa hoja zao katika seneti kuhusu ufujaji wa pesa za kaunti na upande mwingine wanatetea magavana washukiwa mahakamini.

"Inahujumu kazi ya seneti ya kulinda raslimali za kaunti. Seneti haifai kuonekana kupendelea yeyote. Kile wananchofanya kumtetea Sonko mahakamni ni kuonyesha mapendeleo," alisema.

Sakaja alisema kwamba kesi nyingi za ufisadi zimeripotiwa katika kaunti ya Nairobi na huenda zinahusishwa na Sonko na kwa hivyo hana budi ila kujitetea mahakamani.

"Watu wa nyadhifa za juu serikalini wanafaa kujua kwamba siku za kuvunja sheria bila kujali zilipita," alisema.