Sakata katika idara ya Magereza! Ripoti ya uhasibu yafichua

prisons
prisons
Uozo katika idara ya magereza ambao huenda uligharimu mtoa ushuru shilingi bilioni 1.8 katika sakata unoayokaribiana na ile ya NYS umefichuliwa na ripoti ya uhasibu.

Ripoti iliyotolewa na mhasibu mkuu wa serikali Edward Ouko yaonyesha vile idara hiyo ililipa wafanyibiashara hewa, kulipia baadhi ya huduma na bidhaa mara mbili na kununua nguo gushi za kujikinga dhidi ya risasi.

Ripoti hiyo ya uhasibu inajiri miezi michache tu baada ya Tume ya kitaiafa ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC ) kufichua jaribio la kufyonza shilingi bilioni 4.8 kupitia kandarasi hewa za usalama na maafisa wakuu wa idara ya magereza na katika idara ya usalama wa ndani.

Malipo haya yalitekelezwa wakati Isaiah Osugo alipokuwa kamishna wa magereza wadhifa aliohudumu kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya kustaafu. Mahasibu kwa mfano, waligunduwa kwamba shilingi milioni 304.4 zilizolipwa kutoka makao makuu ya magereza kwa ununuzi wa chakula hazipatikani kuambatana na stakabadhi katika magereza.

Katika ulipaji mwingine unaotiliwa shaka, Ouko aligundua kwamba wafanyibiashara wawili waliolipwa shilingi milioni 2.4 kwa kusambaza bidhaa Katika gereza la Kibos hawakusambaza chochote.  Kulingana na ripoti, maafisa wakuu wa magereza jijini Nairobi walituma shilingi milioni 12.4 kulipia madeni ya gereza la Kisumu lakini pesa hizo hazikuwafikia wafanyibiashara waliokuwa wametoa huduma.

Kuhusu zabuni ya kuwekwa kamera za CCTV katika gereza la Naivasha, Ouko anasema kumesheheni ukiukwaji wa kanuni za utoaji zabuni na kupelekea kupotea kwa shilingi bilioni 1.7.  Anasema hata ingawa mwanakandarasi alilipwa shilingi milioni 12 kwa madai ya kusambaza kamera 190, walithibitisha kwamba ni kamera 158 pekee zilizowekwa, na kupelekea kupotea kwa kamera 32.

“Ripoti ya uhasibu pia ilibaini kuwa jumla ya kamera 52 zenye thamani ya shilingi milioni 4.2 zilizowekwa katika eneo la mapokezi na eneo la hospitali zimeharibika na kwa hivyo hazifanyakazi,” Ouko alisema.

Ripoti pia ilifichua kwamba mwanakandarasi alisambaza bodi nane za kugawa umeme badala ya 30 na kupelekea kupotea kwa 22 zenye thamani ya shilingi million 550,000.