Sarah Cohen aachiliwa kwa dhamana

Sarah Wairimu mjane wa mfanyibiashara aliyeuawa kinyama Tob Cohen ameachiliwa kwa dhamana.

Wairimu ambaye ndiye mshukiwa mkuu katika kesi ya mauaji ya Cohen aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni mbili.  Jaji Stella Mutuku hata hivyo alimuagiza Sarah kutokaribia kampuni iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu Tob Cohen, Tob Limted.

Kabla ya kuachiliwa, Mahakama pia ilimtaka Wairimu kueleza vile atagharamia maisha yake wakati kesi dhidi yake itakapokuwa inaendelea. Wazazi wake na mtu yeyote ambaye atachukuwa jukumu la kuishi na Wairimu pia wanatakiwa kueleza kwa maandishi kwamba wamekubali kuishi na kugharamia mahitaji yake wakati kesi ikiendelea.

Upande wa mashtaka ulielezea kutoridhishwa kwao na uamuzi wa Sarah kuachiliwa kwa dhamana. Wakili wa Sarah Phillip Murgor hata hivyo alikaribisha uamuzi huo akisema kwamba kuendelea kuzuiliwa kwa mteja wake ni ukiukaji wa haki zake.

Sarah Wairimu ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya Tob Cohen alikanusha mashtaka hayo katika mahakama kuu mbele ya Jaji Stella Mutuku. Inadaiwa kuwa kati ya Julai 19 na 20 Sarah Wairimu alimuua Cohen na kuuficha mwili wake ndani ya tangi la chini ya ardhi.

Mwendesha mashtaka Catherine Mwaniki alikuwa ameomba muda zaidi kuzuiliwa kwa Sarah ili waweka mikakati ya kuwapa ulinzi mashahidi katika kesi hiyo.

Akiwa nje kwa dhamana Wairimu hatoruhusiwa kungia katika boma lao la kifahari na hata kuasiliana na dadake Cohen, Gabriele Cohen na kakake Bernard Cohen.