Sarah Cohen adai kuwepo njama ya kunyimwa mali ya mumewe

Mjane wa bwenyenye Tob Cohen, Sarah Wairimu amekanusha madai kwamba marehemu mumewe alikuwa anadaiwa shilingi milioni 35 na wanasiasa wawili kutoka Kiambu.

Kwenye hati ya kiapo aliowasilisha mahakamani, Wairimu anasema kwamba hakufahamu chochote kama bwanake alikuwa anadaiwa na mtu yeyote kiasi kikubwa cha pesa kama hicho.

Alisema kwamba alipata kujua kuhusu madai haya kwenye vyombo vya habari baada ya kufunguliwa kwa wasia ya Cohen.

“Pia niligundua kwamba hafla ya kufunguliwa kwa wasia ya Cohen ilihudhuriwa na mwanasiasa, Patrick Muiruri na wanasiasa wengine wawili kutoka Kiambu walisema wanamdai Cohen shilingi milioni 35,” hati ya kiapo ilieleza.

Mjane huyo amabye anazuiliwa kuhusiana na mauaji ya mumewe alisema kwamba alisoma kwenye magazeti kuwa hakuachiwa chochote na Cohen katika Wasia yake. Alidai kwamba Gabrielle Van Straten na kakake Bernard Cohen watawasilisha ombi la kutaka wasia hiyo ianze kutekelezwa.

Wairimu alitaka kuachiliwa kwa dhamana ili kumwezesha kupigania haki yake kama mjane na mmiliki mwenza wa mali ya Cohen. Katika hati ya kiapo, Wairimu anasema hakuna sababu ya kutosha yeye kunyimwa dhamana akishikilia kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa mahakamani kumhusisha na mauaji ya mumuwe.

Anashtumu shemeji zake kwa kushirikiana ili kuhakikisha asiachiliwe kwa dhamana na mahakama.

“Nimeshangazwa na kushtushwa na hatua ya dadake marehemu mume wangu Gabrielle Van Straten na wakili Chege Kirundi kusisitiza kufunguliwa kwa wasia hata kabla ya kuzikwa kwa mumewangu na nikiwa korokoroni,”alihoji.

Wairimu anasema kwamba lengo ni kuhakikisha ananyimwa haki zake kisheria kwa mali na urithi wa marehemu mumewe. Alidai kwamba mkurugenzi wa idara ya upelelezi nchini George Kinoti anafanya juu nchini kuwakabidhi kifunguo cha nyumba yake watu waliotajwa katika wasia bila hata kufuata taratibu za kisheria.

“Baada ya kufunguliwa kwa wasia ya mume waingu, Gabriele na mumewe hawakuwa tena na faida na Tob Cohen na wakaondoka nchini licha ya wao kusema hadharani kwamba walitaka kumfanyia Cohen mazishi ya heshima chini ya tamaduni za kiyahudi,” alidai.

Hati hiyo ya kiyapo itasikizwa mahakamani baada ya Sarah kukubali au kukataa mashtaka.