Sarakasi: Jinsi mgonjwa alivyotoroka kutoka hospitali baada ya upasuaji

Ng'ang'a
Ng'ang'a
Palizuka sarakasi katika mahakama ya Kibera baada ya mkuu wa oparesheni katika hospitali ya Nairobi Women alipoonyesha kanda ya video ya mgonjwa akitoroka hospitalini bila kulipia huduma za matibabu.

Ng'ang'a alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kupokea huduma na kuhepa kulipa Januari 10,2017.

Katika kanda ya video iliyowasilishwa kortini Jumanne, Stanely Ng'ang'a ambaye alifanyiwa upasuaji wa mguu anaonekana akichechemea na mikongojo akitoka nje taratibu.

Tena anaonekana akizungumza na Gabriel Otieno ambaye ni mlinzi kabla ya kuelekea lango la kutoka nje.

Pia hao wawili wanaonekana wakizungumza kwa muda kabla ya Otieno kumsindikiza  Ng'ang'a kutoka hospitalini kupita eneo la Annex 48.

Jumanne, mkuu wa oparesheni wa hospitali Daniel Were aliiambia korti kuwa Ng'ang'a alikuwa amezuru hospitalini mara tatu na kutumia kadi ghushi ya KRA ili kupata matibabu inayogharimu shilingi 962,000

"Mara nyingi alikuwa akitumia kadi ya matibabu ya mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini - KRA kupata matibabu hapa, lakini leo hana bahati," Were aliambia hakimu mkuu wa mahakama Barbara Ojoo.

Alisema kwamba mshtakiwa alirejeshwa tena hospitalini mara ya pili Februari 18 na kuhudumiwa na daktari Mogire.

Kulingana na Were, mshtakiwa alitoroka hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji kwa usaidizi wa Otieno.

"Tafadhali Ng'ang'a fikiria tena vizuri, umekujia matibabu sio matembezi tu muulize daktari Mogire aliyekuhudumia, gharama ya matibabu yako ilikuwa juu," korti iliambiwa.

Shahidi kutoka KRA Fatuma Mohamed alisema kuwa alipokea simu ya Erick Gitonga kutoko hospitali ya Nairobi Women ambaye alimwambia amsaidie mfanyakazi wao kulipa ada ya matibabu mwaka 2017.

Fatuma alisema kwamba aliarifiwa kuwa mgonjwa alikuwa amerejea tena hospitalini lakini alikuwa na deni la awali.

Gitonga hufanya kazi katika kitengo cha kushughulikia madeni na huduma kwa mkopo.

"Je kamera za CCTV hutumiwa kuona jinsi wezi huiba hospitalini au kuzuia wizi? Ng'ang'a aliuza.

Lakini Were alimjibu kuwa kamera hizo hutekeleza kazi hizo mbili.

Aidha Ng'ang'a aliendelea kuuliza idadi ya kamera za CCTV, tarakilishi, na idadi ya wafanyakazi katika chumba cha oparesheni za kamera hizo na iwapo kamera hizo zilikuwa zimeunganishwa na king'ora pamoja na umbali wa chumba hicho kutoka lango kuu.

Mshtakiwa huyo alitaka kujua iwapo hospitali hiyo ina kamera za IP pamoja na vifaa vingine lakini Were alidinda kujibu.

"Rafiki yangu siwezi kukuambia mambo hayo fiche, unataka kujua ili uje kuibia hospitali baadaye ?" Were alimjibu.

Ng'ang'a alishangazwa na jinsi upasuaji wa jeraha dogo mguuni hugharimu kiasi hicho na alimwagiza kutoa sababu.

"Je una maanisha kuwa kulazwa kwangu siku iligharimu maelfu ya pesa, una maana kuwa malazi hugharimu shilingi 88,00?" Ng'ang'a aliuliza.

Lakini Were alimjibu kuwa bili ilipanda juu kwa kuwa hakuwa na ruhusa ya daktari kuondoka.

Jaji aliyekuwa akisikiza kesi hiyo aliagiza iangaziwe tena Januari 20

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO