Saratani ya Korodani na ile ya koo zaongoza katika kuangamiza wanaume - Kenya

SARATANI
SARATANI
NA LUKE AWICH

Taasisi ya kitaifa ya Saratani imechapisha ripoti inayoeleza viwango vya maradhi ya saratani katika kila kaunti, hatua ambayo taasisi hiyo inasema itachochea serikali kubuni sera mwafaka kukabili ugonjwa huu.

Ripoti hiyo ambayo imewasilishwa kwa kamati ya bungeni ya Afya na afisa mkuu mtendaji wa taasisi hiyo Alfred Kiragu imeweka peupe aina za saratani zinazo waathiri wanaume na wanawake katika baadhi ya kaunti nchini.

Kulingana na ripoti hiyo saratani ya koo na ile ya korodani zinaongoza katika maambukizi ya satarani miongoni mwa wanaume katika kaunti 11 zilizoorodheshwa.

Kaunti hizo ni: Nairobi, Kisumu, Meru, Mombasa, Kakamega, Kiambu, Nyeri, Nakuru, Bomet, Embu na Eldoret.

Saratani ya koo au ya umio ndio inayoongoza nchini na kuna visa vingi vya saratani hiyo katika kaunti za Kisumu, Kakamega, Nyeri, Nakuru, Bomet na Eldoret, ikiathiri wanaume na wanawake kulingana na taasisi ya kensa nchini.

Saratani ya matiti inaongoza miongoni mwa wanawake katika kaunti hizo teule 11.

Kulingana na ripoti hiyo, maambukizi ya kensa ya matiti ni mengi mno katika kaunti za Nairobi, Meru, Mombasa, Kiambu, Nakuru na Embu. Katika kaunti ya Nairobi wanaume wengi waonakabiliwa na hatari ya kuugua saratani ya korodani kwa asilimia 32.1 ikifuatwa na ile ya umio kwa asilimia 12.8.

Saratani ya utumbo ni ya tatu katika maambukizi katika kaunti ya Nairobi kwa asilimia 10.3.

Saratani ya matiti ndio hatari zaidi miongoni mwa wanawake katika kaunti ya Nairobi kwa asilimia 37.4 ikifuatwa na ile ya uzazi kwa asilimia 23.7 huku saratani ya umio ikiwa ya tatu kulingana na ripoti ya taasisi ya kitaifa ya saratani NCI.

Wanaume wengi katika kaunti ya Kisumu wanahatari ya juu kuugua saratani ya koo au umio kuliko saratani nyingine kulingana na utafiti uliyofanywa. Katika eneo hilo lililoko karibu na ziwa Victoria maambukizi ya ugonjwa huo ni asilimia 9.9 huku saratani ya korodani ikichangia asilimia 7.

Wanawake katika kaunti ya Kisumu kwa upande mwingine wanakabiliwa na hatari ya juu kupata saratani ya uzazi kuliko saratani yoyote ile kulingana na takwimu. NCI inaweka maambukizi ya sarani ya uzazi kwa asilimia 15.6 ikifuatwa na saratani ya matiti kwa asilimia 11 huku ile ya koo ikiwekwa katika asilimia 8.6.

Katika kaunti ya Meru, saratani ya korodani ni ya juu miongoni mwa wanaume ikifuatwa na ile ya koo na kisha ya tumbo. Mombasa kensa ya korodani ni tishio kubwa kwa wanaume ikifuatwa na ile ya kinywa na kisha ya umio ikiwa katika nafasi ya tatu.

Wanawake wa pwani wanakabiliwa na hatari ya juu kupata saratani ya matiti. Saratani ya uzazi ni ya pili huku ile ya koo ikiwa ya tatu. Kila mwaka Kenya husajili takriban visa vipya 47,887 vya saratani na takriban vifo 32,987 kutokana na maradhi ya saratani.