Serikali yakanusha kuwa kesho ni likizo ya kumsherehekea Kipchoge

Wizara ya usalama imekanusha madai kuwa kesho ni likizo ya umma, kwa heshima ya Eliud Kipchoge. Katika mtandao wa twitter wizara hiyo jana iliwataka wakenya kupuuza picha iliyokua na notisi ya gazeti la serikali iliyokuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Hayo yakijiri, mfanyibiashara Jimi Wanjigi amepuuzilia mbali ujumbe kwenye mtandao wa Twitter ambao umekua ukisambazwa kwamba atamzawadi ndege bingwa Eliud Kipchoge.

Hata ingawa Wanjigi amempongeza Kipchoge kwa mafanikio hayo makubwa, amesema akaunti hio ya twitter ni ghushi.

Ifuatayo ni msururu wa mkusanyiko wa habari humu nchini,

Msafara wa magari ya kampeni ya mwaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra Macdonald Mariga ulivamiwa jana na gari moja kuharibiwa. Mbunge wa Lang’ata Nixon Korir amekishtumu chama cha ODM kwa kuhusika na mashambulizi hayo. Mariga ameahidi kuwa ataendelea na kampeni zake.

Wadau wa sekta ya afya kaunti ya Taita Taveta wameanzisha kampeni ya hamasa dhidi ya maradhi ya fistula. Mwanagaenokolojia wa kaunti hiyo Deepak Parmar anasema watu wengi wenye maradhi ya fistula wanapitia unyanyapaa, wakikosa kujitokeza kutafuta matibabu. Katika kampeni hiyo ya mwezi mmoja, wagonjwa watafanyiwa upasuaji bila malipo na kupewa mafunzo mengine ya afya ya uzazi.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya amewahakikishia wakaazi na wakulima kuwa kiwanda cha sukari cha Mumias kitafufuliwa na kuanza kufanya kazi tena. Oparanya amewasuta baadhi ya viongozi kwa kuchangia kudorora kwa hali ya kiwanda hicho.