Serikali yapuuzilia mbali madai ya Tangatanga kwamba Huduma Namba itatumiwa kwa njama za kisiasa

Kangi
Kangi
Serikali imepuuzilia mbali madai ya wabunge wa mrengo wa tangatanga kwamba kuna njama ya kutumia Huduma Namba kisiasa mwaka 2022.

Katibu mwandamizi katika wizara ya usalama wa ndani Moffat Kangi siku ya Ijumaa alisema kwamba hakuna njama yoyote fiche katika usajili wa Huduma Namba na kuwataka wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kuhusu suala hilo.

Siku ya Alhamisi wabunge wanaomuunga mkono naibu rais na ambao walikuwa wameandamana naye katika mkutano kaunti ya Kajiado walidai kuwepo kwa njama ya kuvuruga data kupitia Huduma Namba kwa sababu za kisiasa.

Wabunge hao walidai kwamba watalaam walikuwa wameajiriwa kusimamia awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba.

“Mbona idara ya NIS inahusishwa katika mapendekezo ya usajili badala ya wizara husika ?” aliuliza seneta wa Nakuru Susan Kihika.

Kihika alisema kwamba wito wa kufanyika kwa awamu ya pili ya kuwasajili wakenya kwa Huduma Namba ni utapeli, kama tu sakata ya coronavirus ambapo mabilioni ya pesa za walipa ushuru zilifujwa.

“Wakenya wamechoka na serikali hii fisadi. Hii ndio sababu tunaunga mkono kuvunjwa kwa bunge kama alivyoshauri Jaji Mkuu,” Kihika aliongeza.

Lakini akijibu madai hayo katibu mwandamizi wa usalama wa ndani Moffat Kangi alisema kwamba lengo kuu la kusajili wakenya katika Huduma Namba ni kuimarisha huduma za serikali kwa wananchi wake.

Mbunge wa Kimilili Didmus Baraza alikuwa amesema kwamba nchi haiwezi kuendelea kupoteza pesa wakati huu ambapo wakenya wengi wanapitia wakati mgumu kiuchumi.

“Pesa nyingi zilitumika katika awamu ya kwanza ya usajili wa Huduma Namba. Hatuwezi kuendelea kupoteza pesa kwa miradi ambayo haina manufaa kwa umma,” Barasa alisema.

Serikali imetanza kufanyika kwa awamu ya pili ya kusajili wakenya kwa Huduma Namba.

Soma habari zaidi hapa;