Shujaa Mugabe alikuwa nguzo ya harakati za ukombozi barani Afrika - Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta hapo jana aliomboleza kifo cha aliyekuwa Kiongozi wa Zimbabwe Robert Mugabe kwa kumtaja kuwa shujaa wa harakati za ukombozi barani na kiongozi mashuhuri aliyejitolea kupigania hadhi ya Waafrika.

Rais alisema kiongozi huyo mwanzilishi wa Zimbabwe iliyo huru atakumbukwa daima kwa mchango wake katika harakati za ukombozi wa mataifa mengi ya Afrika ambayo yalinufaika kutokana na usaidizi wa shujaa huyo wa mali na maarifa katika miaka ya 80 na 90.

“Marehemu Shujaa Mugabe alikuwa nguzo ya moyo wa Uafrika, alitoa usaidizi mkubwa na umoja kwa mataifa mengi ya Afrika katika harakati zao za ukombozi kumaliza utawala wa kikoloni na ubaguzi wa rangi,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alizungumza katika Uwanja wa Kitaifa wa Michezo wa Rufaro jijini Harare nchini Zimbabwe, alipojiunga na viongozi wengine ulimwenguni na kanda pamoja na maelfu ya raia wa Zimbabwe wakati wa mazishi ya Robert Gabriel Mugabe ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 95 katika hospitali moja nchini Singapore wiki iliyopita.

Alisema Rais huyo wa zamani kila mara alikuwa akijali maslahi ya Wafrika na hakusita kupigania umiliki na utumizi bayana wa rasilimali za Afrika kwa manufaa ya raia wake.

“Marehemu Rais Mugabe ameacha alama ya kudumu katika historia ya Zimbabwe na bara la Afrika kwa ujumla, kupitia msimamo wake thabiti na ari ya ukombozi wa kisiasa na kiuchumi,” kasema Kiongozi wa Kenya.

Rais Kenyatta, ambaye alikuwa ameandamana na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, alisema katika maisha yake yote Shujaa Mugabe aliendelea kutoa changamoto kwa Afrika kusimama kidete na kujipa nafasi na sauti katika jamii ya mataifa.

“Kama Kiongozi wa Kiafrika na msomi maarufu, alikuwa na msimamo imara kuhusiana na harakati za bara la Afrika za kusuluhisha changamoto zinazolikabili. Hakusita kusisitiza kwamba matatizo ya Afrika yanahitaji suluhisho za Kiafrika,” kasema Rais.

Rais Kenyatta aliwasihi viongozi wa Afrika kusimama imara na kupigania maslahi ya bara hili kwa heshima ya mashujaa wake wa ukombozi, akisema hii ndio njia pekee ya kuwaenzi ipasavyo viongozi wa Afrika waliofariki.

“Ni wajibu wetu kudumisha matumaini hayo na kutimiza ndoto hizo za Afrika huru yenye maendeleo,” kasema Rais akiongeza kwamba licha ya kutengwa na wengine kutokana na imani yake katika harakati za kuiendeleza Afrika, Mugabe alidumisha uhusiano wake wa kikazi wa karibu na wenzake barani Afrika.

Kwa heshima ya marehemu Mugabe, Rais alitoa wito kwa viongozi wa bara hili kutahadhari dhidi ya athari potovu na kutumiwa vibaya jambo ambalo huathiri maadili ya kawaida na matarajio ya ukombozi na ustawi wa kijamii na kiuchumi.

“Kama viongozi wa Kiafrika, sharti tuendelee kupigia debe maslahi ya bara la Afrika kama heshima ya kudumu kwa marehemu Shujaa Mugabe na mashujaa wengine waliofariki ambao walipigania ukombozi wa kisiasa na kiuchumi,” kasema Rais.

Viongozi wengine wa Afrika waliozungumza wakati wa mazishi yaliyojawa na simanzi ni mwenyeji, Rais Emerson Mnangagwa, Theodore Obiang Nguema wa Equatorial Guinea na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini pamoja na Marais wastaafu Jerry Rawlings wa Ghana na Sam Nujoma wa Namibia mtawalia.

Rais Mnangagwa alimtaja Mugabe kuwa mwanamapinduzi, mzalendo na kiongozi wa kitaifa aliyezingatia moyo wa Kiafrika unaolenga kuwapa raia uwezo kabla ya maslahi mengine ya kibinafsi.

“Hii leo, Afrika Kusini inaomboleza kifo cha kusikitisha cha kiongozi aliyekuwa katika mstari wa mbele, leo bara la Afrika linatoa machozi, likiomboleza kufuatia kifo cha mtetezi wa Wafrika. Nchi yetu inaomboleza, eneo letu linaomboleza na bara letu linaomboleza, zaidi ya yote familia imepata pigo na inaomboleza," kasema Rais Mnangagwa akiomboleza mtangulizi wake.

Alidokeza kwamba marehemu mwanzilishi wa taifa la Zimbabwe alikuwa msomi maarufu, mwenye fikira endelevu, mwalimu na zaidi ya yote Mwafrika wa kweli ambaye alilinda maslahi ya bara la Afrika kwa kuzungumza kwa niaba ya waliokuwa wakidhulumiwa.

Rais Ramaphosa, aliyeomba radhi kutokana na misururu ya mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni nchini mwake hivi maajuzi, alisema mashambulizi hayo hayafai kwa umoja wa Afrika.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alitoa hakikisho kwamba Serikali yake inatekeleza mikakati kabambe kuhakikisha watu wote wanaendelea kuishi katika mazingira ya amani ya kudumu na utulivu.

Kama sehemu ya sherehe za Kiserikali za kumuaga mwenda zake ambaye alikuwa Kiongozi wa taifa, alipigiwa mizinga 21 pamoja na ndege za kijeshi kupaa angani kama saluti kamili ya kijeshi ya Rais.

Marehemu Mugabe aliyezaliwa mwaka wa 1924 na kuanza kazi akiwa mwalimu aliyehitimu na kupanda ngazi kwenye harakati za ukombozi wa 1980 na baadaye kuongoza Zimbabwe kwa miaka 37 akiwa Rais mwanzilishi hadi mwaka 2017, atakumbukwa na wengi kutokana na hotuba zake nzito na za kusisimua.

Akiwa muumini wa dhati wa Kanisa Katoliki, mzungumzaji mchangamfu na mwanasiasa mwenye mawazo huru, marehemu Mugabe amemuacha mjane, Bi. Grace Mugabe na watoto watatu – Bona, Robert Jnr na Chatunga Bellermine.

-PSCU