Shule kufunguliwa Januari mwaka ujao, hakuna mitihani ya KCPE na KCSE mwaka huu-Magoha

kcpe
kcpe
Shule za msingi na upili zitafunguliwa Januari mwakani huku vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zikitarajiwa kufunguliwa kwa awamu, ametangaza waziri wa Elimu George Magoha.

Magoha amesema kalenda ya mwaka huu ya elimu imefutiliwa mbali kwa sababu ya janga la virusi vya corona. Amesema  wanafunzi wote watasalia katika madarasa waliomo mwaka  wa 2021.

" Kwa ushauriano na wizara ya afya  tumekubaliana kwamba shule zifunguliwe  endapo visa vya covid-19 vitapungua  kwa siku 14 mfululizo. Kuwatenga wanafunzi ndio jambo muhimu la kuzuia usalama wa wanafunzi wote," amesema Magoha .

" Usafiri wa wanafunzi kutoka kaunti moja hadi  nyingine utasababisha changamoto kubwa kwani kuna hatari ya maambukizi ya juu.Tunafurahia kuwaarifu wakenya  kwamba rais amekubali mapendekezo hayo".

Amesema vyuo vikuu vitafunguliwa tu endapo vitaafikia mahitaji yaliyotolewa na wizara ya afya pamoja na ile ya elimu.

Taasisi zote zitafanyiwa ukaguzi  ili kuamua iwapo zinafaa kufunguliwa baada ya kutimiza masharti yote.

Katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion amesema  walihusishwa katika mchakato mzima wa  kuyatoa maamuzi hayo na wanaunga mkono kila hatua iliyochukuliwa na waziri Magoha .

Mhariri: Davis Ojiambo