Si feki!!! Familia iliosafirisha jeneza tupu yasema mazishi yalikuwa ya ukweli

Jumamosi waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema kuwa waliwanasa jamaa wawili waliokuwa wanasafirisha jeneza tupu kwenda kaunti ya Homabay  wakidai wanaenda kuhudhuria mazishi ya jamaa wao.

Familia hiyo ilijitokeza na kusema kuwa mazishi hayo yalikuwa ya ukweli licha ya dereva kupatikana na virusi vya corona.

Kagwe alisema familia hiyo ilifaulu kupita vizuizi vyote kutoka Nairobi kwa kuwasilisha idhini feki na jeneza tupu wakidai walikuwa wanasafiri kuhudhuria hafla ya mazishi.

Hata hivyo nduguye dereva Charles Juma akizungumza na runinga ya NTV Jumapili alikiri na kusema kuwa mazishi hayo hayakuwa feki bali yalikuwa ya ukweli.

"Tulikuwa na jamaa wetu kwa jina Milton Obote ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta. Familia iliamua kuwa ahamishwe hadi kijijini ili kujaribu njia tofauti ya matibabu lakini alifariki nyumbani." Juma Alisema.

Juma alisema kuwa pesa zilichangwa kutoka kijijini na kumtumia mmoja wa jamaa wao aliyekuwa Nairobi kununua jeneza la mwendazake.

Alisisitiza na kusema kuwa idhini ya kusafiri kutoka kaunti ya Nairobi ilikuwa feki huku akidai walifuata sheria zote kupata idhini hiyo.

Akizungumzia suala la ndugu yake kupatikana na virusi alisema kuwa alitengwa katika taasisi moja katika kaunti ya Homabay na huenda ripoti kuwa ndugu yake ana virusi hivyo ni uongo.

"Hatuna vifaa vya kupima COVID-19 Homa Bay, mahali karibu ambapo vipimo vinafanywa ni KEMRI katika kaunti ya Kisumu kilomita kadhaa kutoka Homa Bay, itachukua saa 24 kabla ya kupata matokeo

"Wacha tusifanye makosa sawia na ya Siaya ambapo tunawapa watu ugonjwa na kisha kuwazika haraka ili kufunika ukweli." Alisema Juma.

Kwa sasa, serikali ya kaunti inawasaka waliohudhuria mazishi hayo ili kupelekwa karantini, lakini je, kati ya familia hiyo na waziri wa afya Mutahi nani anasema ukweli kuhusu tendi hilo?

Je ni nani anacheza mchezo wa paka na panya?