'Siasa ni mchezo mchafu, hufilisisha' akiri mbunge Sankok

Sankok
Sankok
Mbunge maalum wa chama cha Jubilee David Ole Sankok, anafichua kwamba atastaafu mapema kutoka ulingo wa kisiasa. Anasema kwamba kiti alichokalia cha ubunge kimekuwa na joto jingi sana na hawezi kustahimili tena. 
"Kabla ya kuteuliwa kuwa Mbunge, nilikuwa na raha mstarehe, ninajutia kuwa Mbunge. Siwezi kuhudumu katika muhula mwingine tena. Njia rahisi ya filisika katika taifa hili ni kuwa mwanasiasa," Sankok alisema.
Yeye adai kukabiliwa na wakati mgumu ambapo raia humuendea na kila aina ya matatizo wakitarajia msaada kutoka kwa kiongozi.
"Siasa za Kenya ni ngumu sana. Ni mchezo mchafu ambao kila mmoja anafikiri kwamba una deni lake. Mimi sikuzoea kupeana vitu vya bwerere. Kama mlemavu, nimeng'ang'ana kimaisha. Sitapeana pesa kiholela " Sankok akiri.
 
Utamgundua Mbunge huyu kwa umbali kutokana na mazoea ya kuvalia suti zinazong'aa huku mara nyingi zikiwa zimechorwa mistari ya rangi ya bendera, alieleza masaibu yake tangu ateuliwe kuwa  Mbunge.

Sankok mwenye umri wa miaka 41, anaelekeza macho yake kwenye umoja wa mataifa kama mshauri mkuu kuhusu maslahi ya walemavu. Anaamini kwamba atachangia zaidi katika shirika hilo ikizingatiwa rekodi ya utendakazi wake katika kipindi alichohudumu kama Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Walemavu.

"Kunao wananchi wengi ambao huamka kila kuchao na kuwasaka Wabunge popote walipo kwa madhumuni ya kupata pesa na hususan Mbunge kama mimi ambaye ninajulikana sana kwa mavazi yangu." Sankok alisema.

Kwa wale wanasiasa ambao hawatoi hela kwa raia, Sankok anasema kwamba huwa wanasutwa sana katika mitandao ya kijamii kwa kuwa na "mikono ghamu". 

Mnamo Agosti 25, 2017 David Ole Sankok aliidhinishwa na IEBC kuwa Mbunge maalum katika chama cha Jubilee ili kuwakilisha  masalahi ya walevamu bungeni.

Sankok  anasema  kwamba amemwarifu Rais Uhuru Kenyatta kwamba hangependa kusalia katika ulingo wa siasa tena. Anadai kwamba anataka 'kujishughulisha na masuala mengine.'