Solskjaer tajilaumu iwapo Man United haitapigania taji - Matic

matic
matic
Nemanja Matic anasema Ole Gunnar Solskjaer atajilaumu iwapo Manchester United haitapigania taji la ligi kuu ya Primia.

Matic, aliyewasili Old Trafford kutoka Chelsea mwaka wa 2017, amecheza dakika 22 tu msimu huu baada ya kucheza mara moja kama nguvu mpya dhidi ya Southampton.

United, ambao walishinda taji hilo mara ya mwisho mwaka wa 2013, wako katika nafasi ya 8 kwenye jedwali baada ya mechi nne na wako nyuma ya viongozi wa ligi Liverpool kwa alama saba.

Hayo yakijiri, Gareth Bale amekiri kwamba hana furaha mwanzoni mwa msimu wa mwaka 2019/20, kufuatia misukosuko ya msimu wa uhamisho ambapo alikaribia kuondoka Real Madrid.

Azma ya mchezaji huyo wa miaka 30 ya kutaka kuhamia timu ya Jiangsu Suning ya ligi kuu ya Uchina ilisambaratika huku kukiwa na ripoti kuwa alikosana na Zinedine Zidane. Bale, ambaye mkataba wake ugani Bernabeu unakamilika mwaka wa 2022, anasema hana furaha kwenye klabu hio ya Uhispania.

Kwingineko, Uhispania ilihitaji juhudi za dakika za mwisho kutoka kwa kipa wa Chelsea Kepa Arriza-balaga ili kuweka rekodi yao ya asilimia 100 katika kundi F katika mechi za kufuzu kwa dimba la Euro. Kepa alimzuia mshambulizi wa Reading George Puscas, Uhispania iliporekodi ushindi wake wa kwanza huko Romania. Sergio Ramos aliwaweka Uhispania mbele kabla ya kiungo wa Borussia Dortmund Paco Alcacer kusawazisha.

Katika habari zingine za soka ya ughaibuni, Diego Maradona ameteuliwa kama kocha mkuu wa klabu ya Argentina Gimnasia kwa mkataba wa hadi mwishoni mwa msimu huu. Uteuzi huo utampelekea Maradona mwenye umri wa miaka 58 kurejea kwa nchi yake kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2010.

Gimnasia kwa sasa wanashikilia mkia katika ligi ya Argentina Primera.