Soma risala ya mwaka mpya wa 2019 kwa wakenya iliyotolewa na Rais Kenyatta akiwa ikulu ya Mombasa

uhuru2019newyearmessage1
uhuru2019newyearmessage1
Hamjambo Wakenya wenzangu

Bila shaka mwaka huu unaomalizika umekuwa wa matukio ya kipekee kwa taifa, familia na jamii.Tunamshukuru Mungu kwa Neema yake, ambayo anatupa bila kikomo hata wakati hatustahili kuipata.

Sawa na kila Mkenya, nawashukuru  ndugu, marafiki na wasamaria wema na hata wale ambao mbeleni hatukutarajia kwa kutushughulikia na kwa kutusaidia.

Kwa niaba ya Serikali na familia yangu, nawatumia salamu za kheri njema nikiwatakia mwaka mpya wa 2019 wenye furaha, salama na wenye mafanikio..

Wakenye Wenzangu,

kamwe Wakenya hawastahili kuhofia maisha yao kwa sababu ya siasa. Kufuatia siasa kali za migawanyiko na uchaguzi wa muda mrefu mwaka jana, tulifikia kiwango cha kuwa na siasa za migwanyiko na tetesi. Wakenya walipoteza maisha na  riziki za mamilioni ya watu kuvurugwa huku biashara zikiathirika kutokana na machafuko.

Tulidhihirisha ukuu wetu kama wananchi tulipoamua kuafikiana miezi mitatu baada ya kuingia  mwaka wa 2018, tukasalimiana tukiwa viongozi, jamii na pia kama raia.

Mbeleni ulimwengu ulituangalia ukiwa na wasiwasi kuhusu uthabiti wetu lakini baadaye uliridhika kwa kufurahia vitendo vyetu vya nia njema na uzalendo. Hatua tuliyochukua kuwaunganisha Wakenya sasa imebadilika kuwa funzo kwa nchi nyingi, zikiwa tajiri na hata zile maskini, ambazo siasa zao zinatishia kuwagawanya raia wao. Ninajivunia binafsi maafikiano; na ninajivunia zaidi mamilioni ya Wakenya ambao wamehakikisha wameiga kitendo cha viongozi wachache katika kuafikiana kwa salamu na tabasamu miongoni mwao.

Amani na utulivu uliotokana na  hatua hiyo inasaidia uchumi wetu kuanza kujithibiti na kurejesha uzingativu wa maendeleo kwa ajili ya Wakenya. Ni dhahiri kwamba maono yetu ya ufanisi wa kibinafsi, familia na hata kama taifa hautaweza kuafikiwa pasipo umoja.

Hivyo basi , namhimiza kila raia wa Kenya, biashara, Mashirika yasio ya kiserikali, Vyama vya Akiba na Mikopo, Makanisa na Misikiti yajitolee kuchukua hatua thabiti na muafaka kuimarisha msingi wa umoja wetu. Nawahimiza muafikiane, muanzishe mipango ya kijamii na kitamaduni ambayo itawaleta pamoja Wakenya bila kujali kabila, rangi, dini au mahali mtu atokako.

Wakenya Wenzangu,

Katika mwaka wa 2018 pia tulijifunza kwamba Kenya inaheshimiwa sana na jamii ya kimataifa.  Hapa nchini tunajitokeza  na mawazo yenye uwezo wa kubadilisha ulimwengu. Maandalizi yetu ya kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu Matumizi ya Raslimali za Majini kwa Ustawi wa Uchumi ni bayana ya mifano ya mawazo hayo.

Katika kongamano hili la kipekee, karibu kila serikali ya ulimwengu iliwakilishwa wakiwemo maelfu ya wanasayansi, waekezaji na watafiti, wote wakimiminika jijini Nairobi kuratibu mpango mpya wa nafasi na ufanisi kwa ulimwengu. Hatua hiyo itasaidia kubuni mamilioni ya nafsi za kazi kote ulimwenguni huku nyingi ya nafsi hizo zikibuniwa hapa nchini Kenya kupitia ongezeko la uekezaji na mawasiliano yaliotokana na kongamano hilo.

Hatua ya maafikiano ya upatanishi na utulivu wa kijamii hapa nchini imekaririwa katika maongozi yetu ya kigeni na kushirikishwa katika mataifa ya nje. Tunajenga uhusiano thabiti na wenye manufaa na Marekani, Uchina, Japan, Muungano wa Ulaya na  majirani wetu; wote wakitambua thamani ya ufungamano wetu inatokana na ukakamavu wa uwezo wetu wa kuunganisha na kutupilia mbali tofauti miongoni mwetu.

Hata ingawa tuko mbali kuafikia uwezo wetu, tunajivunia kwamba Kenya sasa ni taifa lenye uzuri katika ulimwengu. Uwezo wa kuwa nguzo ya wema na ukarimu kwa jamii ya kimataifa, hatua hiyo pia inadhihirishwa kwa uwezo mkuu na wanajeshi wetu shupavu na hodari wanaohudumu katika  harakati za kudumisha amani na kuimarisha utulivu katika  sehemu mbali mbali za ulimwengu.

Tunawashukuru kwa kujitoa  kwao mhanga hatua ambayo imeifanya nchi hii na eneo nzima kuwa salama hata ingawa ni gharama kubwa kwa taifa na bila shaka kwa wanajeshi wetu binafsi. Endapo utamuona mwanajeshi yeyote tafadhali chukua muda kuwashukuru kwa kujitoa kwao mhanga na kuwahudumia wanadamu.

Mwaka huu wa 2018, magaidi waliendelea kuimulika Kenya na Wakenya lakini hawakufua dafu kutokana na  kuzuiwa na kuvurugwa kwa njama zao. Vikosi vyetu vya usalama vimeendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa umakini. Ufanisi wao mkubwa zaidi unatokana na hatua ya raia kuendelea kushiriki nao habari walizo nazo huku wengine wakichukua hatua za kukomesha na kuzima kabisa sifa za magaidi miongoni mwa makundi yasiobahatika ambayo yanalengwa kusajiliwa na magaidi.

Nikiwa Rais wenu, namshukuru kila mwanamume na mwanamke ambaye ametekeleza jukumu katika kampeini ya kitaifa dhidi ya visa vya ghasia za kigaidi.

Katika mwaka wa 2019, namhimiza kila Mkenya kokote aliko awe mwangalifu. Hebu toa habari kwa maafisa wanaohusika ukiona mtu yeyote unayemshuku kijijini au katika eneo unaloishi. Hebu watambue walio karibu nao na kamwe usiwaruhusu magaidi au wahalifu kujificha miongoni mwetu. Kila raia anahitajika kulinda taifa, jamii na familia  zetu.

Wakenya Wenzangu,

Tuna kila sababu ya kujivunia kuwa Wakenya. Mwaka wa 2018 tuliendelea kudhihirishia ulimwengu kwamba tuko na baadhi ya watu wenye vipawa vya kipekee duniani.  Sisi na hata ulimwengu mzima kwa mara nyingine tulitazama kwa mshangao huku Eliud Kipchoge akijibidiisha zaidi ya ilivyotarajiwa kuvunja rekodi ya ulimwengu katika mbio za masafa marefu. Wanariadha wengine wa kiume na wa kike wa Kenya pia walivunja rekodi katika riadha. Tulishangilia ufanisi wa timu ya taifa ya soka ya Harambee Stars, ikihitimu kwa michuano ya Kombe la Mataifa Bingwa Barani Afrika, kwa mara ya kwanza baada ya miaka kumi na mitano ambapo Kenya imekuwa ikishiriki.  Kile walicho nacho wanaspoti hawa wote ni talanta, nidhamu na ukakamavu.

Wengi wetu hatutawahi kuvunja rekodi za ulimwengu katika riadha ama kucheza raga ya kulipwa ama michuano ya ndondi za kimataifa. Lakini tunaweza kuzingatia nidhamu na uvumilivu ambao utaweza kufanya talanta zetu kunawiri. Nakusihi ufanye mwaka wa 2019 kuwa mwaka wako wa kutia bidii ili kuyafikia malengo yako. Kila Mkenya ambaye anaafikia lengo lake la kibinafsi iwe ni kwenye elimu, katika biashara ama maisha ya familia, huwa anaikuza Kenya.

Katika mwaka wa 2018, Serikali ya Kitaifa and zile za kaunti zilidhihirisha kwamba tunaendelea kupata ufahamu wa dhati kuhusu ugatuzi na uwezo wake wa kuimarisha nchi. Naipongeza kila serikali ya kaunti kwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, na nazisifu zile serikali za kaunti ambazo zilitia juhudi kuunga mkono Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo, na sekta zingine muhimu kama vile usambazaji maji, usafi, kuendeleza elimu ya msingi na ile ya chekechea, na kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Wakenya wenzangu,

Mwaka uliopita, tulijifunza kwamba tukiwa wananchi tunaweza kufanya kazi pamoja katika kupigana na ufisadi. Hivi sasa, watu wanaotuhumiwa na uhalifu wa kiuchumi hawawezi tena kutumia kabila kama kisingizio kwa matatizo yao ya kibinafsi. Shukran ni kwa siasa zetu za umoja ambazo zimewafanya washukiwa wa uhalifu wasipate nafasi ya kujificha na wanalazimika kubeba msalaba wao.

Ili kudumisha kasi hiyo, katika mwaka wa 2019 tutaendelea kutia bidii katika kuchunguza na kuwafungulia mashtaka wafisadi. Wakati huo huo, tutachukua hatua mwafaka kurekebisha sera zetu and mifumo ya usimamizi wa fedha za umma ili kufunga njia zozote zinazotumiwa na wahalifu kufuja raslimali za umma.

Zaidi ya hayo, Serikali yangu itaimarisha kazi ya Shirilka la kutwaa  Mali ya Umma  ili kuhakikisha tunapata vibali vya Koti kufunga akaunti za benki na kutwaa mali kama vile magari na majumba. Wale watakaoshtakiwa na makosa ya ufisadi hawataruhusiwa kutumia mali walioipata kwa njia ya haramu huku kesi zao zikiendelea kotini. Mara tu mshukiwa atakaposhtakiwa, mali hizo zitahamishwa kwa Hazina ya Kutwaa  Mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu, ili kutumika katika miradi itakayoimarisha maisha ya Wakenya.

Kushinda vita dhidi ya ufisadi kunahitaji sisi sote tufanye kazi pamoja kama Wakenya huku tukizingatia kwamba ufisadi ni adui wetu sote. Kwa hiyo, namhimiza kila Mkenya kukataa rushwa, na wale wanaojaribu kununua hisani yetu kwa kutumia pesa zilizopatikana kwa njia haramu. Kwa moyo huo huo, vitengo vyote vya serikali lazima vijitolee kushirikiana pamoja dhidi ya adui huyu wa maendeleo.

Kufikia hapo, lazima niseme naridhishwa na kazi ya timu ya mashirika mbalimbali ya serikali, ambayo imehakikisha kwamba udanganyifu katika mitihani ya kitaifa unakomeshwa kabisa katika mfumo wetu wa elimu. Navihimiza vyuo vikuu pia viweke mikakati mwafaka kuhakikisha udanganyifu katika mitihani hautokei katika taasisi hizo. Lazima tumalize visa vya ufisadi katika mfumo wetu wa elimu ili kuhakikisha Kenya inarudisha hadhi yake kama nchi inayotoa elimu bora na ya ushindani mkubwa ulimwenguni.

Wakenya Wenzangu,

Tumeanza utekelezaji wa Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo, ujenzi wa nyumba bora za gharama ya chini, utoaji huduma za afya kwa wote, kujitosheleza kwa chakula na lishe bora, na utengenezaji bidhaa ili kubuni nafasi za kazi kwa vijana wetu. Katika mwaka wa 2019 tutaanza kutekeleza elimu ya msingi na ya sekondari bila malipo na ya lazima inayohakikisha kuwa asilimia 100 ya wanafunzi wanakamilisha masomo yao.

Shule zitakapofunguliwa hapo tarehe 3 Januari, wanafunzi gredi moja hadi tatu wataanza kupata mafunzo kupitia mtaala-endelevu unaozingatia uwezo wa watoto. Matayarisho ya mtaala huu yatapangwa vizuri katika mwaka wa 2019, na natarajia kwamba maafisa wanaohusika na jukumu hili muhimu watatia bidii na kudumisha mawasiliano mema huku tukiendelea kuwakuza viongozi wa kesho.

Pia natoa wito kwa vyuo vyote, ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu, kutoa mafunzo na ujuzi ambao utawawezesha wanafunzi wanaohitimu kuajiriwa na kuwa watu wenye maadili mema ya kikazi. Tunataka Wakenya wapate ujuzi ambao utawawezesha kushindana vilivyo ulimwenguni na waweze kupata kazi kwa urahisi wanapohitimu masomo yao.

Wakenya Wenzangu,

Ningependa kila mjasiriamali na kila mtu anayeendesha biashara ndogo ndogo wajue kwamba hao ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu. Hatujafanya mengi kama inavyohitajika lakini katika mwaka wa 2019, nawaahidi kwamba Serikali yangu itafanya kila juhudi kuwawezesha kukuza biashara zenu kwa urahisi. Tutaangalia sera zote za serikali, ikiwa ni pamoja na ushuru, sheria na kupatikana  kwa mikopo ili kuwawezesha kuzingatia teknolojia ya kisasa ambayo itaimarisha biashara zenu.

Tukijumuisha Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo na kuimarisha biashara ndogo ndogo, marekebisho ya elimu, na mwamko mpya wa siasa zetu za umoja na kubiliana na ufisadi, tunaiweka nchi yetu katika mkondo ufaao katika kuafikia malengo yetu ya kijami na kiuchumi ya Ruwaza ya Kitaifa ya mwaka wa 2030. Tukiwa Wakenya, hakuna tunachohitaji zaidi kuliko kumaliza umaskini kabisa.

Raia wenzangu, hebu mwaka wa 2019 uwe mwaka wa kuafikiana, kuleta nidhamu na uvumilivu katika juhudi zetu. Hebu tuheshimiane na kufurahia tofauti zetu na kuzitumia kuthibiti uraia bora zaidi. Hakuna Mkenya ambaye anaweza kuishi pekee yake, akiwa amejitenga au ametengwa kutoka kwa mahitaji na shauku za raia wengine nchini.

Ukiwa umepanga kufanikiwa kibinafsi, panga kwa njia ya uaminifu. Hebu ufanisi wako usikufaidi wewe pekee  bali pia uwanufaishe wale walio karibu nawe.

Hebu mwaka wa 2019 uwe mwaka wa ufufuzi na uhuisho wa kitaifa;  mwaka ambao tutamwagilia maji mbegu zilizopandwa miaka iliyopita ili zichipuke na  kukomaa kama mti thabiti na mkubwa; mti ambao matunda yake ni mengi na yanayofurahiwa na kila Mkenya.

Kwa heshima na kwa unyenyekevu, nikiwa Rais wa Jamhuri,nawatakia Wakenya wote na ndugu na dada kote ulimwenguni, mwaka mpya wa furaha na mafanikio.

Asanteni na Mungu aibariki Jamhuri ya Kenya.