Sonko aagiza kuboreshwa barabara tatu zaidi jijini Nairobi

Barabara tatu zaidi katikati mwa jiji la Nairobi zinatarajiwa kuimarishwa kama njia moja wapo kupunguza msongamano jijini.

Hii ni baada ya gavana Mike Sonko kuagiza idara ya barabara na uchukuzi kuboresha barabara tatu katikati mwa jiji baada ya kufanikiwa kwa ukarabati wa barabara ya Luthuli Avenue. Barabara hizo tatu ni Banda Street, Accra Lane nyuma ya Accra Street na Gedi Lane.

“Mpango wa kuondoa misongamno katikakti mwa jiji utaendelea kwa utaratibu ili kubuni mazingira bora ya kufanyia biashara kwa wawekezaji na wageni wetu,” Sonko alisema.

Sonko pia amewaonya vikali wanakandarasi wanaopewa kazi na kaunti ya Nairobi dhidi ya kufanya kazi duni.

“Hatutafanya barabara moja mara mbili. Luthuli inafaa kusalia katika hali nzuri kwa angalau miaka 10 kabla ya kufikiria tena kuifanyia ukarabati. Hii inamaanisha kwamba kazi yenu inafaa kuwa ya hadhi ya juu, hii inahusu hata barabara zingine zote,” Sonko alisema.

Waziri wa barabara na uchukuzi Hitan Majevdia amefichua kwamba gavana aliagiza kukarabatiwa kwa kwa barabara hizo tatu ili kupunguza msongamano jijini. Kaunti ya Nairobi inaendelea na mipango ya kukabili misongamano katikati mwa jiji, huku awamu ya kwanza ikiwa kuinua hadhi ya barabara ya Luthuli na kuibadili iwe ya mkondo mmoja.

Asilimia 90 ya ukarabati wa barabara hiyo umekamilika na gavana Sonko ataizundua hivi karibuni.

Majevdia amesema kwamba matatu zinazotumia barabara za Banda Street, Accra Lane na Gedi Lane kutoka katikati mwa jiji zitalazimika kutafuta njia mbadala wakati barabara hizo zikikarabatiwa.