Sonko akamatwa na maafisa wa DCI Voi akiwa kwa SGR

Gavana wa Nairobi Mike Sonko amekamatwa na maafisa wa DCI saa chache baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kutoa amri ya kukamatwa kwake. Sonko alishikwa katika eneo la Voi akiwa safarini kuelekea Mombasa akitumia gari moshi la SGR.

Sonko na washukiwa wengine 16 wanakabiliwa na mashtaka kadha ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Hajji aliagiza kukamatwa na kushtakiwa kwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko. Haji alisema ana ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka ya ufisadi Sonko pamoja na maafisa wa wengine wa idara ya utoaji zabuni.

Sonko na maafisa wengine wa kaunti ya Nairobi wanadaiwa kutumia udanganyifu kulaghai pesa za kaunti. Haji alisema ilikuwa vigumu kupata ushahidi dhidi ya washukiwa kwani baadhi ya maafisa walipokea vitisho na stakabadhi muhimu za kufanikisha uchunguzi kufichwa.

DPP alisema washukiwa walikwa wametumia vijana kuwatisha maafisa wa usalama waliokuwa wakitekeleza majukumu yao. Uchunguzi dhidi ya Sonko ulitekelezwa na tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC, na ushahidi kuwasilishwa kwa DPP ili kumfungulia mashtaka gavana huyo na washukiwa wenzake.

"Nimeagiza kukamatwa mara moja na kushtakiwa kwa gavana Sonko na maafisa wengine kwa madai ya kupokea pesa kutoka kwa kaunti ya Nairobi akiwa anahudumu kama gavana, kujipa mali ya umma kinyume na sheria, ulanguzi wa fedha na makosa wengine ya kiuchumi," Haji alisema.

Mwezi Oktoba, EACC ilianzisha uchunguzi dhidi ya madai ya ufisadi ya ufisadi katika kitengo cha utoaji zabuni na malipo ya jumla ya shilingi milioni 196 katika ujenzi wa Uwanja wa michezo wa Dandora.

Uchunguzi huo ulitokana na mapendekezo ya mamlaka ya utoaji zabuni za umma iliyotilia shaka shuguli ya utoaji wa kandarasi hiyo.