Spurs waoneshwa kivumbi, West Ham yakabwa na Man City

spurs
spurs
Kevin de Bruyne alisaidia na kufunga bao moja Manchester City walipowanyuka West Ham 2-0 katika mechi yao ya kwanza tangu kupigwa marufuku ya miaka miwili na UEFA.

Marufuku hio imewekea wingu hatma ya klabu hio, lakini ikaibua hisia kali miongoni mwa mashabiki wake. Mashabiki walisikika wakiisuta UEFA katika kipindi cha kwanza huku wakibeba mabango ya kuikashifu huku wakiimba nyimbo za kumuunga mkono meneja Pep Guardiola.

Madai kua Manchester City ilikiuka kanuni za kifedha za Uefa si ya ukweli, kulingana na afisa mkuu Ferran Soriano. Mabingwa hao wa ligi ya Premier walipigwa marufuku ya miaka miwili na kutozwa faini ya Uro milioni 30 Ijumaa iliyopita.

Uamuzi huo utalingana na rufaa iliyowasilishwa kwa mahakama kushughulikia masuala ya spoti. Soriano anadai hakuna pesa iliyowekezwa kwenye klabu hio, ambayo haikuwekwa wazi.

Tottenham wana kibarua kigumu ili kuweka matumaini yao ya ligi ya mabingwa hai, baada ya kucharazwa bao 1-0 na RB Leipzig katika mkondo wa kwanza raundi ya 16.

Spurs ambao hawana huduma za Son Heung Min ambaye amevunjika mkono na Harry Kane, walifungwa na klabu hio ya Bundesliga ambayo ilionyesha kuboreka.

Kipa Hugo Lloris ndiye aliyewaokoa Spurs kwa kuzuia mikwaju ya Leipzig kabla ya Timo Werner kufunga kunako dakika ya 58. Kwingineko Atalanta iliwalaza Valencia 4-1.

Msururu wa habari za michezo;

Mkufunzi wa Chelsea Frank Lampard ataelekezewa darubini kali ikiwa klabu hiyo itashindwa kufuzu kwa Champions League msimu huu. Kwingineko Manchester City inamtaka winga wa Bayern Munich Serge Gnabry mwenye umri wa miaka 24, kama sehemu ya mpango utakaomwezesha Leroy Sane, kujiunga na klabu hiyo ya Bundesliga.

Ole Gunnar Solskjaer anasema haijabanika iwapo Marcus Rashford atakuwa sawa kuregea kabla ya msimu kukamilika na ameonya kuwa huenda akakosa michuano ya Euro 2020.

Rashford hajacheza tangu mwezi Januari baada kuumia mgongo wakati wa mechi yao dhidi ya Wolves ya kombe la FA. Kiungo huyo amefungia United mabao 19 msimu huu. Solskjaer alidinda kutoa hakikisho lolote mwezi Januari kwamba Rashford angeregea kabla ya msimu kuisha akisema ingechukua angalau wiki 6 kabla aweze kuanza mazoezi.

Bondia wa timu ya taifa Beatrice Akoth ana matumaini ya kuiwakilisha Kenya kwa mara ya kwanza, katika michuano ya kufuzu kwa Olimpiki jijini Tokyo mwaka huu, inayoandaliwa leo jijini Dakar, Senegal. Akoth, anayepigana kwa uzani wa featherweight amelalamikia joto kali lililoko jijini Dakar, lakini akasema ana muda wa kutosha kulizoea. Nahodha wa timu hio Nick Okoth, msaidizi wake Elizabeth Andiego na bondia Rayton Okwiri pia wanashiriki mashindano hayo.

Matokeo ya kujiondoa kwa Kenya Power kama mdhamini wa sare za Western Stima yameanza kuiathiri pakubwa klabu hio. Stima imethibitisha kuwa mdhamini huyo amewaagiza kusitisha mikataba ya wachezaji, ikitaja ukosefu wa fedha za kulipa mishahara na marupurupu yao. Klabu hio pamoja na Nairobi Stima na Coast Stima, walipata pigo kubwa mwezi uliopita baada ya kampuni hio kutangaza kuondoa udhamini wao.