Tanga Hama : Washirika zaidi wa DP Ruto wamkimbilia Raila

Naibu Rais William Ruto/File
Naibu Rais William Ruto/File
Naibu wa rais William Ruto amepata pigo jingine baada ya washirika wake  watatu muhimu kuiacha kambi yake na kujiunga na mrengo wa rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Watatu hao ni katibu msimamizi wa wizara ya ardhi Gideon Mung’aro,  mbunge wa Laikipia kaskazini  Sarah Korere  na mfanyibiashara wa pwani  Suleiman Shahbal.  Wote walikuwa katika afisi za Raila za Capital Hill ili kutangaza misimamo yao kujiunga na mrengo wa rais na bwana Odiga huku wakijitenga na kundi la tanga tanga. Wa kwanza kuvuka  laini na kujiunga na upande wa pili ni mwakilishi wa akina mama wa Laikipia  Catherine Waruguru. Korere  wakati mmoja alikuwa mtetezi sugu wa DP Ruto  na kauli zake za pingamizi dhidi ya sera za rais Kenyatta na azama ya kisiasa ya Bwana Odinga zinafahamika na wengi. Pia amekuwa mksoaji mkubwa wa mwafaka wa handshake kati ya rais Kenyatta na Odinga.

Alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Jubilee waliolengwa na shoka la kutimuliwa kutoka kamati za bunge lakini sasa amejitokeza na kutangaza kwamba anaunga mkono mwafaka wa handshake  na  BBI. Alikuwa ameandamana na seneta wa  Narok Ledama  ole Kina  alipotangaza kujiunga na mrengo wa Uhur-Raila Kutoka kundi la tanga tanga.

“ Nimempokea mbunge wa Laikipia North  Sarah Korere ambaye ameunga mkono  jitihada za kuliunganisha taifa’ Raila aliandika katika twitter muda mfupi baada ya  kukutana na mbunge huyo.

Tangu chama cha Jubilee kiwafurushe viongozi wa  seneti na bunge waliokuwa katika mrengo wa Ruto kutoka nafasi za uongozi, baadhi ya wabunge kutoka mrengo wake wamekuwa wakizingatia kubadilisha misimamo kisiasa ili waweze kuepushwa na shoka la kuonyeshwa mlango. Gazeti  la The Star limeripoti kugundua kwamba  wabunge wengi wanaomuunga mkono Ruto ambao wanalengwa kuondolewa katika kamati za bunge wanapanga kukutana na Raila  wiki zijazo .

Ruto Ruto amesalia kimya tangu shoka kuwakuta washirika wake  Kithure Kindiki  wa Tharaka Nithi, Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, Susan Kihika wa  Nakuru, Benjamin Washiali wa Mumias mashariki na  Cecily Mbarire(Mteule). Raila  pia amekutana na  mwanasiasa wa pwani CAS Mung'aro  na Shahbal  ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ‘maendeleo ya eneo la pwani’.