TANZIA: Mlipuko wa bomu waua watu 63 harusini

harusi
harusi

Bomu limelipuka katika ukumbi wa harusi katika mji mkuu wa Afghanistan , Kabul na kuwaua takriban watu 63 na kuwajeruhi zaidi ya 180.

Walioshuhudia waliambia BBC kwamba mlipuaji wa kujitolea muhanga alijilipua wakati wa sherehe hiyo ya harusi.

Mlipuko huo ulitokea mwendo wa saa nne na dakika 40 saa za Afghanistan katika eneo lililopo magharibi mwa mji ulio na rai wengi Waislamu wa dhehebu la Kishia.

Kundi la Taliban limekana kwamba ndilo lililohusika na shambulio hilo. Hakuna kundi jingine lolote lililokiri kutekeleza shambulio hilo.

Wapiganaji wa Kiislamu kutoka Dhehebu la Sunni , ikiwemo Taliban na kundi la wapiganaji wa Islamic State mara kwa mara wamekuwa wakiwalenga Waislamu wa Hazara wa dhehebu la Shia walio wachache nchini Afghanistan na Pakistan.

Ni nini tunachojua?

Waziri wa maswala ndani nchini Afghanistan amethibitisha vifo hivyo saa chache baada ya bomu hilo kulipuka .

Picha zilizosambazwa katika mitamndao ya kijamii zilionyesha miili ikiwa imetapakaa huku viti na meza zikiwa zimependukia.

Harusi za Afghanistan huruhusu mamia ya wageni ambao hukongamana katika kumbi kubwa ambapo wanaume hutengwa na wanawake na watoto.

Mgeni mmoja kwa jina Mohammad Farhag alisema kwamba alikuwa katika eneo la wanawake wakati aliposikia mlipuko mkubwa katika eneo la wanaume .

''Kila mtu alikimbia nje akipiga kelele na kulia'', aliambia chombo cha habari cha AFP.

''Kwa takriban dakika 20 ukumbi huo ulikuwa umejaa moshi . Karibu kila mtu katika eneo la wanaume ni aidha wamekufa au kujeruhiwa. Sasa saa mbili baada ya mlipuko , wanaendelea kutoa miili ndani ya ukumbi huo''.

Muhudumu mmoja wa chakula , Sayed Agha Shah alisema kwamba kila mtu alikuwa akikimbia baada ya mlipuko huo.

''Wahudumu wetu kadhaa walifariki ama kujeruhiwa'', aliongezea. Msemaji wa Taliban alisema kuwa kundi hilo linashutumu shambulio hilo.

''Hakuna haki ya shambulio la kusudi kama hilo na mauaji ya kiholela yaliowalenga wanawake na watoto'', Zabiullah Mujaheed alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Nini kilichotokea awali?

Mlipuko huo unajiri siku 10 baada ya bomu kubwa kulipuka nje ya kituo cha polisi cha Kabul na kuwaua watu 14 huku 150 wakijeruhiwa.

Kundi la Taliban limesema kuwa lilitekeleza shambulio hilo.

Siku ya Ijumaa ndugu mmoja wa kiongozi wa Taliban Hibatullah Akhundzada aliuawa kutokana na bomu lililotegwa ndani ya msikiti karibu na mji wa Pakistan wa Quetta.

Hakuna kundi lolote kufikia sasa lililokiri kutekeleza shambulio hilo.

Duru za kijasusi kutoka Afghanistan zinadaiwa kukaribia kutangaza makubaliano ya amani.

-bbc