Tazama wimbo mpya wa Divock Origi baada ya kupatia Liverpool ushindi

Ni siku chache baada ya mshambulizi matata wa Liverpool, Divock Origi kufungia Liverpool bao la ushindi katika kombe la ubingwa wa ulaya dhidi ya Tottenham, lakini sifa bado zazidi kumiminika kutoka dunia nzima.

Origi ambaye ni mwanawe Mike Okoth ambaye alikuwa mshambulizi wa timu ya taifa ya Harambee Stars amekuwa na kampeini ya kufana sana baada ya nyota yake kuonekana kudidimia msimu uliopita.

Mshambulizi huyo alijiunga na Liverpool mwaka wa 2014 ambapo mchezo wake haukuridhisha kocha, Jurgen Klopp na akatumwa katika klabu ya Wolfsburg kwa mkopo ili kunoa makali yake.

Msimu huu ulipoanza, Origi hakupewa fursa ya kucheza mechi za kwanza mbili na habari zikaenea kuwa alikuwa tayari kuondoka timu hiyo. Hata hivyo ripoti zilikiri kuwa Origi alikataa uhamisho wowote na aliamua kusalia Liverpool ili apiganie nafasi yake.

Miezi kadhaa baadaye, jina la Origi ndilo linalosifika zaidi katika maeneo ya Merseyside kwani mabao yake machache ndio yalikuwa muhimu mno katika msimu mzima.

Origi alifunga bao la ushindi katika mechi ya Merseyside Derby dhidi ya Everton katika dakika ya 90+6, kijana huyo wa Mike Okoth pia alifungia Liverpool bao la ushindi dakika ya 86, dhidi ya Newcastle ushindi uliowapa Manchester City tumbo joto.

Isitoshe, mshambulizi huyo wa miaka 24 alifunga mabao mawili dhidi ya Barcelona mechi ambayo waliandikisha historia na kuwapeleka katika fainali za mabingwa wa Uropa.

Siku ya fainali, huku Liverpool ikiongoza kwa bao lake Mo Salah dhidi ya Spurs, mashabiki wa Liverpool walikuwa wamejawa na woga mwingin kwani walihitaji bao lingine ili kuwahakikishia ushindi.

Kijana wa Mike Okoth ambaye aliingizwa uwanjani katika kipindi cha pili, alifunga bao la ushindi huku mechi ikiwa imesalia dakika tatu pekee na kuhakikisha Liverpool wamenyakua taji ambalo limewakwepa tangia mwaka wa 2005.

Kufuatia ushujaa wake, mashabiki wa Liverpool sasa wametunga wimbo spesheli wa kumsifu Origi huku wengi wakiomba apewe kandarasi ya maisha kwa kuwapa msimu wa kufana.

Pata kuskiza wimbo huo katika kiungo kifuatacho.

And now Divock Origi gets the big one! 🔴🔴🔴🔴