The new Wolves? Wazito FC wapo tayari kutetemesha msimu mpya wa KPL

Klabu ya Wazito FC inatarajiwa kurejea kwenye ligi kuu msimu ujao baada ya kushushwa daraja msimu wa 2019 huku mechi yao ya kwanza ikiwa ni dhidi ya Nzoia Sugar mjini Machakos.

Wazito FC kwa sasa inawatia kiwewe maadui wake wa ligi kuu nchini Kenya Msimu ujao hasa baada ya kuleta sura mpya klabuni hapo.

Mwenyekiti wa Wazito FC, Ricardo Bardoe ameamua kujaza sura za kutisha msimu ujao klabu hapo.

Karim Nizigiyimana

Aliyekuwa mlinzi wa Gor Mahia mburundi Karim Nizigiyimana amerejea nchini Kenya kwa mara ya pili na raundi hii atakuwa anavalia jezi ya Wazito Fc. Nizigiyimana mwenye umri wa miaka 31 anatarajiwa kuongeza nguvu kwenye ngome ya Ulinzi ya Wazito hasa kufuatia wakati huu nahodha wao Gicheru anaugua Jereha.

Nizigiyimana ametokea kuchezea taifa lake la Burundi kwenye michuano ya AFCON kule nchini Misri.

Bernad Ochieng

Kama ilivyo kwake Nizigiyimana,Ochieng pia alishiriki michuano ya AFCON kule misri akiwakilisha taifa lake la Kenya kwenye michuano hiyo. Ochieng anatarajiwa kuleta ushindani wa hali ya juu kwake Gicheru pamoja na wahome kwenye eneo la ulinzi la kati la Wazito Fc.

Abouba Sibomana

Mrwanda Abouba Siboumana alikamilisha uhamisho wake hapo jana hadi klabu ya Wazito akitokea klabu ya APR ya nyumbani kwao Rwanda. Sibomana aliyewahi kukipigia Gor Mahia kama mlinzi wa kushoto anatarajiwa kuongeza tajriba pamoja na ushindi jambo litakaloimarisha matokeo ya timu hio msimu ujao kwenye ligi kuu nchini Kenya.

Elvis Rupia

Mshambulizi huyu amejiunga na klabu ya Wazito akitokea klabu ya Zambia, Power Dynamos. Elvis almaarufu kama 'El Machapo' alikuwa mshambulizi wa Nzoia Sugar na alitupia wavuni magoli 15 kwenye mechi 22 alizochezea Nzoia Sugar. Machapo mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa kuleta ushindani kwenye ngome ya ushambulizi ya Wazito FC.

Mansoor Safi Agu

Agu ni kiungo mshambulizi aliyekuwa anasakatia timu ya taifa ya Uganda kwa vijana wenye umri wa miaka isiyozidi 20. Maansoor anatarajiwa kuongeza nguvu kwenye idara ya kiungo ya Wazito Fc. Amejiunga na wakali hawa akitokea shule ya upili ya Kubuli.

Mkurugenzi wa Wazito FC  Solomon Alubala amesema kuwa klabu hio inajihadharisha na makosa ya klabu ya Fulham ya Uingereza iliyotumia hela nyingi na mwishowe ikaishia kuzama msimu uliofuata.

Solomon anasema kuwa wapo tayari kutetemesha ligi kuu nchini Kenya msimu ujao hasa ikifuatiwa sajili wanazofanya kwa sasa.