Tit for Tat:Mke wangu alitoroka na kakangu,nikamnyakua dadake!

man
man
Geoff Kiplagat  hakujua cha kufanya wakati mke wake  Jebet  alipobadilika asiweze kufahamu kilichokuwa kikifanyika .

Ndoa yao ya miaka 7 sasa ilikuwa hatarini na juhudi zake za kutafuta msaada wa wazazi wa pande zote, viongozi wa kidini na  hata rafiki wao wa karibu hazikuzaa matunda .

 "Alianza ujeuri ambao sikujua ulitokea wapi, alipuuza kila nilichomuambia na sasa ikawa kila mtu anajifanyia mambo yake," alisema  Geoff .

Wiki  mbili  zilizopita walikuwa wamelumbana kuhusu hatua ya Jebet kutaka kujilinganisha kimaisha na jirani zao. Mke wake hakuwa amefahamu kwamba maisha ya kila mtu ni tofauti kwa hivyo alikuwa akimpa presha mume wake kumfanyia vitu ambavyo majirani walikuwa wakiwafanyia  wake zao.

"Kila alipojua mke wa jirani  amenunuliwa nguo na mumewe, basi  naye  pia alitaka nimnunulie nguo, hakutaka kujua iwapo nilikuwa na pesa au la," alisema Geoff .

Malumbano yao kuhusu ushindani wa Jebet yalisababisha mgogoro katika ndoa  yao na ikawa vigumu kwa Geoff kumridhisha kwa sababu alivyotaka vilikuwa vingi kwa wakati mmoja na hata vya gharama ya juu ambayo  hangeweza kumudu. Matokeo yake –kununa kila wakati na wakajipata wanalala katika vyumba tofauti .

Hata hivyo , Geoff anakumbuka kwamba kuna kitu alichoshuhudia lakini hakukiwaza sana au kukichukuliwa kwa uzito wakati huo. Kakake mdogo  James alikuwa akija nyumbani kwake kila mara kuwatembelea  yeye na mkewe. Aligundua kwamba mke wake na ndugu yake walikuwa na urafiki mzuri kwa sababu licha ya matatizo katika ndoa yao, Jebet alikuwa akimkaribisha vizuri na kumfanyia maandalizi  James wakati alipokuja kuwatembelea.

Katika fikra zake alijiambia ni mashehemji hao tu hapakuwa na la ziada – Kumbe ngoma ilikuwa ikichezwa!  Usiku mmoja mke wake  akilala , Geoff kwa sababu ya kuwa tu na  shauku alitaka kujua Jebet amekuwa akizungumza na nani kila mara kupitia jumbe za sms na katika whatsapp. Alipoifungua simu ya mkewe alipatwa na mshutuko kugundua kwamba  mke wake alikuwa ameihifadhi nambari ya kakake James kama ‘sweet love’.

Alishangaa mbona  mkewe alikuwa akimuita ndugu yake jina hilo lililoashiria kuwepo uhusiano zaidi wa kindani.  Alikumbuka  jinsi wawili hao walivyokuwa wakiangaliana wakitabasamu tabasamu  kila walipoonana. Hakujali kuhusu gumzo zao wakati huo lakini sasa taswira nzima ya kilichokuwa kikifanyika ilimjia .

Hamaki ilimsakama pale akijiuliza  cha kufanya. Mkewe alikuwa amelala hajui kinachofanyika  lakini Geoff alitamani kumuamsha wakati ule ili apate  majibu  ya maswali yake kutoka kwake. Akaamua kesho atafanya kikao na mkewe ajue ukweli lakini tayari  alikuwa ameshathibitisha hofu yake kwamba kweli mkewe na kakake walikuwa wapenzi.

Geoff alipomkabili mkewe kumuuliza maswali, alipatwa na pigo kwa sababu mkewe hakukana bali alisema ni kweli yeye na James, kaka ya mumewe wamekuwa  katika uhusiano wa kisiri kwa muda sasa. Mke wake aliendelea kumuambia kwamba James alikuwa akimjali sana kwa sababu alifanya kila juhudi za kumpa vitu  alivyotaka.

Wakiendelea kujibizana, Jebet aliingia chumbani akachukua vitu vyake vyote na kuondoka. Alisema hatomrudia mumewe na kwamba wamepanga kuanza maisha upya na  James.

Geoff alisononeka  na kuhisi uchungu wa kusalitiwa na kakake pamoja na mke wake. Aliwaza kuhusu hatua atakayochukua lakini kama  ilivyofanyika baadaye alisema uchungu wake kamwe hautamzuia pia kulipiza kisasi !

Alikumbuka kwamba Jebet alikuwa na dadake, aliyekuwa akimfuata na ambaye wakati mwingi alikuwa akija kuwatembelea. Alikata kauli ya kumtongoza ili awe katika uhusiano naye kama njia moja ya kumkwaza mke wake.

 "Aliamua kutoroka na kaka yangu, mimi sasa nitamchukua dadake ili apate uchungu kama niliyopitia,"  alisema Geoff .

Visa hivyo havikuwafurisha jamaa zao na juhudi za kuwapatanisha hazikuwahi kufua dafu huku Jebet akiendelea kuishi na  kaka ya mume wake naye Geofee akiishi na dada ya mke wake .