Good Friday! 22 wapona virusi vya corona Kenya, watano zaidi waambukizwa

kmut
kmut
NA NICKSON TOSI

Watu 10 zaidi waliokuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona nchini Kenya  wamekuwa wa hivu punde kupona ugonjwa huo na wanatarajiwa kuruhusiwa kurejea nyumbani. Kumi hao sasa wanafikisha 22 idadi ya watu waliopona ugonjwa huo nchini Kenya.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe hata hivyo ametangaza kwamba chini ya saa 24 maafisa wa afya nchini Kenya wamefanyia vipimo watu 504 ambapo kati ya hao watu 5 wamepatikana na virusi vya Corona na kufikisha 189 idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo nchini Kenya.

Kulingana na waziri wa afya Mutahi Kagwe, kati ya watu hao watano, watatu ni wa kike na wawili ni wa kiume.

Visa hivyo vitano vimetokea katika kaunti za Mombasa vikiwa 3, Nairobi 1 na Narok.

Waziri Kagwe aliongeza kuwa maafisa wa afya 5000 waliotarajiwa kuajiriwa na tume ya uajisiri ya serikali ya kitaifa sasa wataajiriwa na serikali za kaunti.

Wakati huo huo maafisa wa afya alfu 100 na madaktari 4000 wameanza kupewa mafunzo ya kuhusiana na namna ya kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

Kagwe vile vile amethibitisha kupokea msaada kutoka taifa la Uchina wa vifaa muhimu ambavyo vinatarajiwa kuongeza idadi ya kufanyia vipimo watu wengi ili kutathmini idadi ya wale walioathirika na virusi hivyo.

Wananchi wametakiwa kuvalia  barakoa  ili kuhakikisha kuwa hakuna kusambaa kwa virusi hivyo na atakayepatikana akiwa hana atachukuliwa hatua.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO