Video ya Ruto akiomba Mama Ngina kumuunga mkono yaibuka

Muhtasari

• Video ya Ruto akimbembeleza mama Ngina Kenyatta kumuunga mkono kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti imevuja mitandaoni, siku moja tu baada ya Ngina kutangaza kumuunga mkono Raila Odinga.

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: Maktaba

Wakenya ni miongoni mwa watu wanaojua kuweka rekodi kwenye makabrasha na hata kuunanisha matukio fananishi hata baada ya zaidi ya miongo kadhaa.

Jumanne, Wakenya waligawanyika katika makundi mawili hasimu ya kisiasa kutokana na kuibuka kwa video ya mama wa kwanza wa taifa, Ngina Kenyatta akimpigia kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga debe huku akiwataka watu kumsikiliza Uhuru Kenyatta na kufuata anachowaagiza katika chaguo la mgombea urais.

Katika video hiyo ambayo Ngina anawarai watu kwa lugha ya Kikuyu, anatafsiriwa akisema kwamba rais wa sasa Uhuru Kenyatta ambaye ni mwanawe hawezi kuwapotosha Wakenya kwa kuwaambia kiongozi anayefaa kumrithi kama rais, huku akionekana kumkashfu naibu rais William Ruto kwa kumpa mwanawe wakati mgumu ndani ya uongozi wa Jubilee.

Sasa Jumatano paliibuka mkanda wa video ambapo naibu rais William Ruto anasikika akijimaliza yake yote kumuomba Mama Ngina kumchukulia kama mtoto wake wa pili na kuwarai watu kumuunga mkono katika uchaguzi wa Agosti 9.

“Nataka nimuulize mama wetu, mheshimiwa Mama Ngina Kenyatta, safari hiyo ingine aliita Uhuru Kenyatta mtoto wake wa kwanza, sasa siku hiyo ingine, unite mtoto wako wa pili kwa sababu niko hapa, nikuje nifanye hiyo ingine ambayo imebaki,” Ruto anasikika akiomba.

Mwanablogu Abraham Mutai ambaye anajulikana na wengi kwa kupinga vikali sera za Ruto amepakia video hiyo akimkumbusha yeye na wenzake kutoka mrengo wa Kenya Kwanza, kwamba wakati mmoja Ruto alitaka Ngina amuunge mkono lakini sasa wamejisahau na kumtupia maneno ya kila aina baada yake kutangaza kumuunga mkono Raila Odinga ambaye ni mpinzani mkubwa wa Ruto kuelekea kivumbi cha Agosti 9.