Kuria avunjika moyo baada ya Janet Mbugua kukataa ombi la kuwa mgombea mwenza wake

Muhtasari

•Kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi (CCK)  amefichua kwamba Bi Janet amekataa ombi lake kutokana na mambo binafsi ya dharura.

•Kuria anatazamia kuwa gavana wa nne wa Kiambu ifikapo mwezi Agosti na atwania kiti hicho kwa tikiti ya CCK.

Moses Kuria na Janet Mbugua
Moses Kuria na Janet Mbugua
Image: HISANI

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ni mwenye huzuni baada ya mtangazaji Janet Mbugua kukataa ombi lake la kuwa mgombea mwenza wake katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Kiambu.

Katika taarifa ambayo alichapisha Alhamisi asubuhi, Kuria amesema kwamba mtangazaji huyo wa habari ndiye aliyependekezwa zaidi kuwa mgombea mwenza wake.

Kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi (CCK)  amefichua kwamba Bi Janet amekataa ombi lake kutokana na mambo binafsi ya dharura.

"Nimevunjika moyo. Baada ya kupata alama za juu zaidi katika utafutaji wa vipaji vya kumpata naibu gavana wa Kiambu, Janet Mbugua hatachukua kazi hiyo kutokana na dharura za kibinafsi zisizokadiriwa ambazo anapaswa kushughulikia mara moja. Utawala wangu hakika utapata njia ya kufaidika kutokana na uzoefu na uwezo wa Janet katika siku zijazo," Kuria amesema.

Mbunge huyo amesema iwapo atanyakua kiti hicho angependa kumshirikisha Janet kwenye utawala wake kwa kuwa ana ushawishi mkubwa kwa vijana, wataalamu na kina mama.

"Janet anawapa msukumo mkubwa vijana, wataalamu, wanawake na kina mama vijana wa nchi hii," Alisema.

Kuria anatazamia kuwa gavana wa nne wa Kiambu ifikapo mwezi Agosti na atwania kiti hicho kwa tikiti ya CCK.