Urbanus Ngengele wa Machakos agura UDA na kuingia Azimio

Muhtasari

• Mwandani wa naibu rais William Ruto, Urbanus Ngengele amegura chama cha UDA na kujiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja.

• Alisema kwamba kwa ushirikiano na viongozi wengine, watahakikisha kwamba jamii hiyo itakuwa ndani ya serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

George Owiti
George Owiti
Image: Urbanus Ngengele

Mwandani wa naibu rais William Ruto, Urbanus Ngengele amegura chama cha UDA na kujiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja.

Alisema kwamba atawania kiti cha ugavana katika kaunti ya Machakos, kupitia chama tanzu chini ya mwavuli wa Azimio.

Ngengele aliwania useneta wa kaunti ya Machakos kwa tikiti ya UDA katika uchaguzi mdogo uliofanyika 18/3/2021 ila akabwagawa na Agnes Kavindu wa Wiper.

Awali alikuwa amezindua rasmi kampeni zake za kuwania ugavana wa Machakos kabla ya kugura Ijumaa.

Alikuwa ameandamana na katibu mkuu wa chama cha ODM kaunti ya Machakos, Domnic Kaleli alipokuwa akiwahutubia wanahabari katika hoteli moja huko Machakos.

“Baada ya kufanya mashauriano ya kina na wafuasi wangu na wakazi wa Machakos, imebainika wazi kwamba eneo hili halitaki kuwa sehemu ya upinzani tena. Hivyo basi ni bora jamii hii ikishirikiana na mrengo ambao utaunda serikali ijayo baada ya kuwa nje serikali kwa zaidi ya miaka kumi,” Ngegele alisema.

Aidha, alisema kwamba alimshirikisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, gavana wa Machakos Afred Mutua, Charity Ngilu wa Kitui na Kivutha Kibwana wa Makueni katika maamuzi hayo.

“Inawadia muda ambao jamii ni kubwa kuliko mtu binafsi nan do sababu leo baada ya mashauriano marefu na viongozi wa Ukambani, nataka kutangaza rasmi kwamba nimejiunga na mrengo wa Azimio la Umoja,” alisema.

Alisema kwamba kwa ushirikiano na viongozi wengine, watahakikisha kwamba jamii hiyo itakuwa ndani ya serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.