"Sikuwa na nia mbaya," Moses Kuria aomba radhi jamii ya Luo

Muhtasari

• Moses Kuria - Kama nilivyosema awali, sina nongwa yoyote na Raila Odinga wala jamii ya Luo. Nilikuwa tu narejelea kiapo cha 1969 ambacho kilitolewa kabla hata ya kuzaliwa kwangu

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria
Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria
Image: Facebook

Mbunge wa Gatundu Kusini hatimaye amezidiwa na shinikizo la cheche kali kutoka baadhi ya Wakenya na kuamua kuweka wazi kuhusu matamshi yake kwamba kinara wa Azimio la Umoja hajatahiriwa.

Kuria ambaye alitoa madai hayo wiki mbili zilizopita kwa kusema kwamba mwaka 1969, jamii ya Kikuyu walilishwa kiapo na rais wa kwanza Jomo Kenyatta kuhusu kutomuunga mkono mtu ambaye hajapitia jandoni, alipokea kashfa nyingi huku baadhi wakitaka tume ya NCIC kumchukulia hatua kwa kile walisema ni madai ya kugawanya wakenya.

Mbunge huyo anayeegemea mrengo wa Kenya kwanza ikiongozwa na naibu rais William Ruto wikendi iliyopita baada ya shinikizo kuzidi, alilazimika kuweka wazi kuhusu matamshi yake hayo na kusema hakuwa anamaanisha kuwatukanisha watu wa jamii ya Luo.

“Kama nilivyosema awali, sina nongwa yoyote na Raila Odinga wala jamii ya Luo. Nilikuwa tu narejelea kiapo cha 1969 ambacho kilitolewa kabla hata ya kuzaliwa kwangu na ambacho maelezo yake yanaweza kutolewa na Kapteni Kungu Muigai, mpwa wa Jomo Kenyatta ambaye nyumbani kwake kiapo kilisimamiwa na babake Kungu James Gitoki Muigai. Mchungaji John Gatu, marehemu Njenga Karume walirejelea kiapo hicho. Kwa wale wote wanaonichafua nasema hivi, hizi ajali za kihistoria zinaeleza mengi sana yanayotokea leo kisha unashangaa kwanini. Kunirushia mawe si jambo la busara. Kujaribu kujifunza kitu kutokana na kile ninachosema kunasaidia zaidi,” aliandik Moses Kuria kupitia ukurasa wake wa facebook.