"Matiang'i saidia!" Esther Passaris alia msafara wake kuvamiwa

Muhtasari

• "Polisi na Matiang’i msafara wetu umevamiwa. Tuko Westlands karibu na Deepsea. Saidia!" - Esther passaris.

Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Image: Facebook

Mwakilishi wa kike katika kaunti ya Nairobi, Esther Passaris alisema Jumatatu kwamba gari refu yeye na timu yake walikuwa wanatumia katika kampeni zake lilishambuliwa mchana peupe na watu ambao alidai wanalitumwa na mpinzani wake.

Passaris alisema kwamba genge hilo la vijana waliolitupia maw na kuliharibu vibaya gari hilo wanajulikana na kumtaka Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i na polisi kutuma vyombo vya usalama katika eneo la tukio.

Mwakilishi huyo wa kike analenga kuwania kipindi cha pili katika nafasi hiyo na alishambuliwa wakati anaendeleza msururu wa kampeni zake katika eneo bunge la Westlands jijini Nairobi.

“Polisi na Matiang’i msafara wetu umevamiwa. Tuko Westlands karibu na Deepsea. Saidia! Genge la wahuni limechukua funguo za gari letu na wanataka pesa ili kurejesha funguo. Tumekwama ndani ya gari letu. Tunawajua wahuni hawa. Wamevunja vioo vya gari. Saidia!” aliandika Passaris kwenye Twitter yake.

Baadae tena mwanasiasa huyo ali-tweet na kusema kwamba vyombo vya usalama vilifika kwa muda na kutuliza hali huku akimshukuru OCS wa Parklands na kamanda wa polisi, Westlands kwa kuchukua hatua ya haraka na kuzuia hali kutokuwa tete.

“Shukrani kwa kamanda wa polisi katika kaunti ya Nairobi James Mugera na OCS kutoka kituo cha Parklands James Murigu kwa kuitikia kwqa upesi na kuchukua hatua dhidi ya wahujumu wetu. Vita na vitisho katika gari la kampeni havifai kuvumiliwa,” alitweet Passaris.