Mapenzi na bangi: Wajackoyah 'adunga luku' ya kirastafari

Muhtasari

• Mgombea urais wakili profesa george Wajackoyah afurqahisha wengi kwqa muonekano wake wa kirastafarian, ambapo anadhihirisha mapenzi yake kwa bangi ambayo ametangaza kuihalalisha akishinda urais.

Wakii profesa George Wajackoyah
Wakii profesa George Wajackoyah
Image: Screenshot, instagram

Mgombea urais katika uchaguzi wa Agosti Profesa George Wajackoyah amewaacha wengi wakizungumza mitandaoni baada ya video yake akiwa amevalia mavazi ya kirastafarian kuvujishwa kwenye mtandao wa Instagram.

Wajackoyah ambaye pia ni wakili wa muda mrefu alipata umaarufu mkubwa mapema mwezi Januari baada ya kutangaza kwamba atawania urais kupitia kwa chama chake cha Roots na kuibua mjadala mkali hata zaidi baada ya kuachia manifesto yake.

Katika manifesto yake, Wajackoyah alisema ajenda kuu ni kuhalalisha matumizi ya bangi ambayo alienda mbele kusema kwamba mauzo ya mumea huo ulioharamishwa katika mataifa mengi ulimwenguni yatatumika kulipa deni la mikopo kutoka taifa la Uchina.

Katika video hiyo ambayo ilipakiwa Instagram na mcheshi Captain Otoyo, Wajackoyah anaonekana ametaradadi katika mavazi hayo maarufu nchini Jamaica huku miguuni akiwa amevalia viatu kama vya kijeshi.

Msomi huyo anayelenga kumrithi rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba pindi atakapoapishwa ataalika wananchi wote katika ikulu ya Nairobi na kuvuta bangi kwa pamoja kama ishara ya kuihalalisha.

Muonekano huo wake umeshabikiwa na kutafsiriwa na wengi kama ishara ya kuonesha mapenzi yake kwa bangi, kwani mavazi kama hayo ni maarufu Jamaica ambapo bangi inatumika kwa wingi mno.