Charity Ngilu amsuta DP Ruto baada ya kusema ana mpango wa kukabiliana na ufisadi

Muhtasari
  • Charity Ngilu amsuta DP Ruto baada ya kusema ana mpango wa kukabiliana na ufisadi
Gavana wa Kitui Charity Ngilu
Image: Musembi Nzengu

Gavana wa Kitui Charity Ngilu amemsuta Naibu Rais William Ruto baada ya kusema kuwa ana mpango wa kina wa kukabiliana na ufisadi nchini iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Katika chapisho la Twitter, akijibu matamshi ya Ruto kama ilivyonukuliwa na gazeti la Star, gavana huyo alisema kuwa Naibu Rais amekiri kujua zaidi kuhusu ufisadi kuliko mtu mwingine yeyote.

“Kimsingi amekiri kwamba anaelewa wizi kuliko mtu mwingine yeyote, jambo ambalo halina ubishi,” alisema.

Ruto, alipokuwa akiwahutubia wakazi katika Kaunti ya Wajir siku ya Alhamisi, alisema ni Muungano wa Kenya Kwanza pekee ndio unaweza kumaliza ufisadi nchini.

Alikuwa akimjibu kinara wa chama cha ODM Raila Odinga aliyemshtumu kuwa mzalishaji wa ufisadi.

Ngilu alilinganisha zaidi ombi la Ruto kwa Wakenya kumpigia kura na mbwa mwitu anayeomba kuwaongoza kondoo.

"Mbwa mwitu anaomba kuruhusiwa kuongoza kondoo, Hii Kenya yetu itatuonyesha mambo kweli. Ama tumuwachie mungu?," alisema.

Katika mkutano huo, DP alimshutumu Raila kwa ufisadi na kuahidi kumaliza ufisadi ikiwa atachaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9.

"Huna msingi, huna mpango na kundi pekee lenye mpango wa kupambana na ufisadi ni Muungano wa Kenya Kwanza kwa sababu tutaendesha Hazina ya Mahakama," DP alisema.

Akizungumza Alhamisi wakati wa kampeni zake Kaunti ya Wajir, Ruto alisema serikali yake itatoa fedha za kupambana na ufisadi kwa Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma. (ODPP).

"Tutajenga taasisi za kupambana na rushwa," alisema.