Ruto ana hasira kwa sababu niliungana na Raila - Kalonzo

Muhtasari

• Kalonzo amesema Ruto ana hasira baada yake kuungana na Raila Odinga.

• Amemtaka kukubali kwamba Odinga ndiye atakuwa rais wa tano wa taifa hili.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka amesema kwamba naibu rais William Ruto amekuwa akionyesha wazi kughadhabishwa baada yake kuamua kuungana na kiogozi wa ODM Raila Odinga.

Kalonzo alisema kwamba kitendo cha Ruto kukejeli vuguvugu la Azimio la Umoja katika kampeni zake ni ishara tosha kwamba mrengo wa Kenya Kwanza unahangaika.

Kulingana na Musyoka, naibu rais alishikwa na kiwewe baada ya kuona wazi kwamba Raila Odinga ataibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha kumrithi rais Uhuru Kenyatta.

“Tangu nitangaze kushirikiana na Raila nimekuwa na amani sana. Ni wazi kwamba Raila Odinga ndiye atakuwa rais wa tano wa taifa hili, ndo maana Ruto anaonekana kukasirishwa,” Kalonzo alisema.

Kiongozi huyo wa Wiper alikuwa ameungana na Raila katika kampeni eneo la Turkana mbele ya uchaguzi wa Agosti 9.

Aidha, alimtaka Ruto kukoma kumtupia cheche rais Uhuru Kenyatta na kuheshimu uamuzi wake wa kumuunga mkono Raila Odinga.

Ikumbukwe kwamba awali Kalonzo alikuwa amedinda kushirikiana na Raila Odinga, ila baadaye alilazimika kulegeza kamba baada ya mazungumzo na mashauriano ya muda mrefu.

Je nguvu na ushawishi wa Kalonzo utamsaidia Raila Odinga kumbwaga naibu rais William Ruto?