Jaguar akanusha kulazimishwa na Ruto kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha ubunge

Muhtasari

Mbunge huyo alitaja ripoti kwamba aliagizwa kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho na naibu rais William Ruto kuwa za uongo. 

Kuhusu mazungumzo na Mbugua kuwania kiti hicho, Jaguar alisema: "Mpinzani wangu alikubali mazungumzo katika eneo bunge lake la zamani

Mbunge wa Starehe Charles Kanyi Njagua maarufu Jaguar
Mbunge wa Starehe Charles Kanyi Njagua maarufu Jaguar
Image: Hisani

Mbunge wa Starehe Charles Njagua, almaarufu Jaguar, amekanusha ripoti kwamba amejiondoa katika kinyang'anyiro cha kuhifadhi kiti chake cha ubunge. 

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, mbunge huyo alitaja ripoti kwamba aliagizwa kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho na naibu rais William Ruto kuwa za uongo. 

Pia alikanusha kufanya mazungumzo yoyote na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Simon Mbugua na kuafikia kwamba ajiondoe kwenye kinyang'anyiro cha ubunge. 

"Kama Mbunge wa Starehe ningependa kuwajulisha wapiga kura wangu kwamba sijajiuzulu kwasababu ya mgombea yeyote na sijafanya mazungumzo yoyote na Naibu Rais kuhusiana na suala hili," Njagua alisema. 

"Nilichaguliwa na watu wa Starehe na nina mamlaka ya kuwawakilisha. Sitakuwa mshiriki wa mazungumzo yoyote". 

Kuhusu mazungumzo na Mbugua kuwania kiti hicho, Jaguar alisema: "Mpinzani wangu alikubali mazungumzo katika eneo bunge lake la zamani. Starehe mambo ni tofauti Wahome Thuku". 

Alimtaja Wahome Thuku kwa sababu ni miongoni mwa watu waliosambaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba alilazimika kujiuzulu. 

"Charles Kanyi (Jaguar) ameagizwa na mamluki wa Karen kujiuzulu kwa sababu  ya Simon Mbugua kama mbunge wa Starehe. Marafiki zake sasa wanashangaa ni kwa nini na jinsi gani mbunge aliye kwenye kiti  anapaswa kuambiwa aondokee mgombeaji mwingine," Wahome alisema. 

Mbugua ni mbunge wa zamani wa Kamukunji lakini alihamia Starehe kujaribu bahati yake baada ya kupoteza kiti hicho. Kiti cha Kamukunji kwa sasa kinashikiliwa na Yusuf Hassan wa Azimio.