Sakaja kuwania ugavana Nairobi kwa tikiti ya UDA

Muhtasari

• Sakaja amesema yupo tayari kushiriki katika kura za mchujo.

• Amekana madai ya kujiunga na chama cha ANC.

Johnson Sakaja
Johnson Sakaja
Image: Ezekiel Aming'a, KWA HISANI

Seneta wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amejiunga na chama cha UDA kinachoongozwa na naibu rais William Ruto ambapo pia atatumia tikiti ya chama hicho kuwania ugavana wa kaunti ya Nairobi.

Sakaja alisema kwamba aligura Jubilee muda mrefu uliopita na kujiunga na UDA huku akijiandaa kuchukua nafasi ya gavana wa sasa Anne Kananu.

“Sijawahi kujiunga na ANC. Nilipotoka Jubilee nilikwenda moja kwa moja katika chama cha UDA,” Sakaja alisema.

Kauli ya Sakaja imewashangaza wengi ambao walikuwa wamemhusisha seneta huyo na kinara wa ANC Musalia Mudavadi.

Licha yake kumpigia debe Mudavadi kumrithi rais Uhuru Kenyatta, Sakaja anaonekana kubadilisha mkondo wake wa kisiasa.

Duru za kuaminika zinasema kwamba Sakaja na seneta wa Kakamega Cleophas Malala walihusika pakubwa katika mazungumzo yalipelekea ushirikiano kati ya Mudavadi na naibu rais William Ruto.

Sakaja atatoana kijasho na aliyekuwa mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru katika kura za mchujo chamani humo zinazotarajiwa kufanyika Alhamisi wiki ijayo.

Huku naibu rais William Ruto akipambana kuwaunganisha wawili hao, Sakaja anaonekana kushikilia msimamo wake wa kuingia katika kura za mchujo.

Mshindi katika mchujo huo atashindana na wagombea wengine kutoka kwa vuguvugu la Azimio la Umoja katika uchaguzi wa Agosti 9.