"Utapinga hadi lini?" Moses Kuria amsihi rais Kenyatta ajiunge na muungano wa Kenya Kwanza

Muhtasari

•Kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi amemtaka rais Kenyatta,na ambaye ametoka katika eneo bunge lake, kujiunga na muungano wao wa Kenya Kwanza.

Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Image: MAKTABA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ameendelea kumkosoa rais Uhuru Kenyatta kufuatia chaguo lake la upande wa kisiasa.

Katika ujumbe wakewa Jumamosi, Kuria alimdokezea rais  kwamba viongozi wakubwa wa taifa hili wakiwemo maspika wa bunge na seneti pamoja na asilimia kubwa ya wabunge wanaunga mkono muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto.

"Ndugu Rais, Naibu Rais, Maspika wa Seneti na Bunge la Kitaifa, 60% ya Wabunge katika Seneti na Bunge la Kitaifa, zaidi ya 70% ya MCAs kote nchini na mimi mwanakijiji mwenzako na rafiki wa muda mrefu tuko Kenya Kwanza," Kuria alimwambia rais kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi amemtaka rais Kenyatta,na ambaye ametoka katika eneo bunge lake, kujiunga na muungano wao wa Kenya Kwanza.

"Utapinga hadi lini?" Kuria alimuuliza rais.

Ujumbe wa Kuria ulikuja punde baada ya spika wa bunge la Kitaifa kuongoza chama chake cha DP kutia saini mkataba wa muungano na Kenya Kwanza.

Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika hoteli moja jijini Nairobi na ilihudhuriwa na wanasiasa mbalimbali wakiwemo DP Ruto, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang'ula miongoni mwa wanasiasa wengine wanaomuunga mkono naibu rais.

Spika Muturi alisema uamuzi wake wa kujiunga na Kenya Kwanza  ni baada ya kushauriana na wanachama wa chama chake na viongozi wa jamii.

"Nina furaha kwamba baada ya mazungumzo kadhaa kuhusu kuja pamoja, leo tumetambua ndoto hiyo ya kufanya kazi pamoja kwa watoto wetu na watoto wa watoto wetu," Spika Muturi alisema.

Aliongeza: "Nimesafiri katika maeneo mengi ya nchi na ninaweza kuthibitisha kwamba mapigo ya moyo ya Wakenya wengi yanaambatana na matamanio ninayoshikilia katika muungano huu. Tuna furaha kujumuika na muungano huo".

Aliendelea kukemea serikali ya sasa akisema halitalazimisha taifa zima kuelekea mwelekeo fulani wa kisiasa.