(VIDEO) Nataka kuwa mgombea mwenza wa Raila! - Alfred Mutua

Muhtasari

• Gavana Mutua - Najua kwamba pamoja na Raila, atakuwa ananituma na ninakimbia Chap Chap na kutekeleza mambo ili Kenya iwe kama Singapore au Malaysia.

Gavana wa Machakos Dr Alfred Mutua
Gavana wa Machakos Dr Alfred Mutua
Image: Facebook

Gavana anayeondoka madarakani katika kaunti ya Machakos, Dr Alfred Mutua ameibua madai yenye ukakasi mkubwa ambapo sasa anasema kwamba anataka kuwa mgombea mwenza wa Kinara wa vuguvugu la Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Kinara huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap alikuzungumza Jumapili katika mkutano alioitisha na wanahabari alisema kwamba baada ya tathmini ya muda mrefu na kuelewa matakwa na vigezo katika vuguvugu hilo, ameamua pia kutoa pendekezo lake la kutaka kuwa mgombea mwenza na naibu rais wa serikali ijayo ya Azimio, kama muungano huo utaibuka na ushindi katika uchaguzi wa Agosti 9.

“Ninaamini kwamba uongozi wa taifa letu unahitaji uzoefu wa mtu mzima mpiganaji wa haki na demokrasia, ukijumuishwa na nguvu, rekodi ya kimaendeleo iliyodhibitishwa, uwezo na uzingatio wa mtu mdogo mwenye nguvu. Kwa hiyo, kutokana na himizo la wanachama wangu, ninajipendekeza mwenyewe ili kuzingatiwa kama mgombea mwenza katika nafasi ya naiibu rais wa Jakom Raila Amollo Odinga. Najua kwamba pamoja na yeye, atakuwa ananituma na ninakimbia Chap Chap na kutekeleza mambo ili Kenya iwe kama Singapore au Malaysia ambapo watu watakuwa na pesa nyingi mifukoni mwao,” alisema gavana Mutua.

Gavana huyo alisema kwamba anajua fika Raila anataka mtu ambaye anaweza amini na kusema kwamba anamuamini na anajua Raila pia anaweza kumuamini kama mgombea mwenza.

Matamshi haya yanakuja siku chache tu baada ya chama cha Wiper kusisitiza kwamba wanataka Kalonzo Musyoka kuwa mgombea mwenza huku Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui pia akisisitiza kwamba katika muungano wa Azimio la Umoja, watu wa kutokea eneo la Mlima Kenya hawatarajii kiti chochote chini ya unaibu rais!