Moses Kuria: Raila akiwa rais atamgeuka Uhuru, alimfunza rais wa Kongo kumgeuka rais aliyempaisha madarakani

Muhtasari

• Moses Kuria alidai Raila alimfunza rais wa Kongo Tshisekedi kumgeuka rais mtangulizi aliyempaisha uongozini kama mradi wake.

Moses Kuria, William Ruto, Raila Odinga, Uhuru Kenyatta
Moses Kuria, William Ruto, Raila Odinga, Uhuru Kenyatta
Image: Facebook

Siasa za Kenya zinavyozidi kushika kasi na kukolea munyu kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, watu na wachambuzi mbalimbali wanazidi kutoa maoni yao, wengine wakitabiri kipi kitajiri kabla na baada ya matokeo ya uchaguzi huo.

Mmoja kati ya wale wanaozungumza kwa uhuru bila kuzimiwa taa za mchana kama lilivyo takwa la katibu kwa watu kuzungumza bila kuzuiwa, Kiongozi wa Chama Cha Kazi ambaye pia ni mbunge wa Gatundu Kusini anasema kuna uwezekano mkubwa sana wa kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga kumtema rais Uhuru Kenyatta pindi ikitokea kwamba ameshinda kinyang’anyiro cha urais.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook hivi majuzi wakati rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi alipotua nchini ili kutia wino wa mkataba ulioikaribisha Kongo kwenye muungano wa Afrika Mashariki, Kuria aliibua madai kwamba Odinga ndiye alikwenda Kongo kumfunza Tshisekedi jinsi ya kumgeuka mtangulizi wake Joseph kabila aliyemsaidia kuingia madarakani akidhani Tshisekedi atakuwa kibaraka wake.

Kuria alisema kwamba Raila ni mkufunzi mzuri sana wa masuala hayo na yeye anavyochukuliwa na Kenyatta kwamba atakuwa kibaraka wake, atageuka na kubadilisha Ngozi hiyo dhidi ya Kenyatta pindi atakapomsaidia kuingia madarakani kama rais wa 5 wa Kenya.

“Ni Raila Odinga aliyekodisha ndege hadi DRC kumfundisha Felix Tshisekedi jinsi ya kumgeuka Joseph Kabila ambaye ingawa Tshisekedi alikuwa mradi wake. Katika tukio lisilowezekana Raila atakuwa Rais, atamfanyia Uhuru Kenyatta jambo lilo hilo. Kwani Uhuru anadhani atapata 40% ya serikali na Kalonzo 30% na Raila anasalia kugawana 30% kati ya wandani wake wa ODM baada ya kupigania kwa miaka 60 kuwa Rais kati yake na babake? Hata Baba hapangwingwi,” aliandika Moses Kuria.

Matamshi ya Kuria yanakuja siku moja tu kabla ya mwenyekiti wa chama cha Jubilee Kanini Kega kusema kwamba chama hicho hakiamini pakubwa Raila kwa sababu wanahisi kinara huyo wa ODM atakaposhinda atamtafuta William Ruto ili wawe na maridhiano na hivyo kumuacha Uhuru Kenyatta katika upweke.

Kuria anaegemea mrengo wa naibu rais William Ruto na analenga kuwania ugavana wa kaunti pana ya Kiambu kupitia chama chake cha Kazi.