"Nchi imekushinda, bei zimepanda!" Ndindi Nyoro amfokea rais Kenyatta

Muhtasari

• Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amemfokea Uhuru Kenyatta kwa kushindwa na uongozi, kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

Rais Uhuru kenyatta, MP Ndindi Nyoro
Rais Uhuru kenyatta, MP Ndindi Nyoro
Image: State House Kenya, Facebook

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro anadai kwamba nchi ya kenya imekuwa ikimpwerepweta rais Uhuru Kenyatta na hivyo kumshinda katika kuiongoza kama rais.

Nyoro ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook akimshtumu rais Kenyatta kutokana na ongezeko la bei za bidhaa muhimu kama chakula na kawi nchini.

“Hebu tuwe waaminifu kabisa. Rais Uhuru Kenyatta ameshindwa kutawala nchi hii. Hakuna mafuta, hakuna maziwa, hakuna pesa, hakuna chakula. Bei ya juu ya kila kitu kuanzia gesi, unga, chumvi, mchele, sukari, mafuta ya kupikia na kimsingi kila kitu kingine kimepanda bei,” alilalama Nyoro.

Alisema kwamba licha ya Wakenya kuteseka kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizi, kinaya ni kwamba familia ya Kenyatta ndio inashikilia usukani katika biashara nyingi na hivyo wanatabasamu wakielekea kwenye benki huku Mkenya wa chini mlala hoi akizidi kukandamizika.

Alitolea mfano kwamba serikali ya Kenyatta kupitia shirika la maji la WARMA, pia waliongeza bei ya maji kwa mara tatu zaidi na hilo lina maana kwamba kampuni zote za kusambaza maji zitalazimika kuongeza bei hiyo ili kukwepa kutoenda hasara.

“La kusikitisha ni kwamba wanafanya Biashara katika takriban sekta zote na kwa hivyo wanatabasamu hadi kwenye benki (ambayo pia wanamiliki) huku Wakenya wakilia kwa uchungu. Hivi majuzi tu serikali yake kupitia WARMA pia iliongeza ada ya watumiaji wa maji mara tatu - kwa hivyo hata kampuni za maji zitaongeza bili hivi karibuni. Utawala huu usio na uwezo utakumbukwa kama kosa kubwa lililotokea kwa Nchi yetu. Ukweli kwamba wana ujasiri wa kujilinganisha na Rais Kibaki ni tusi kwa Mwana uchumi huyo mkuu na Wakenya,” alisema Nyoro.

Kama hiyo haitoshi, Nyoro alimkejeli Kenyatta kwamba haoni aibu hata baada ya kufanya magumu maisha ya Wakenya, bado anazidi kuwalazimishia kibaraka ambaye ataongoza kwa kulinda mali yake kenyatta na wengine.

 Kibaraka hapa alimaanisha kinara wa ODM Raila Odinga ambaye anaungwa mkono na rais Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 9.

“Na wako bize kusukuma "puppet project" kwa Wakenya ili kuendeleza na kulinda uporaji na kuasisi zaidi state capture!! Hasira kote nchini lazima itafsiriwe katika vitendo hivi karibuni,” alimaliza kwa hasira Nyoro.

Mbunge alikuwa wa Kwanza kuikosoa vikali bajeti iliyosomwa wiki jana na Waziri wa fedha Ukur Yatani kwa kusema kwamba takwimu alizozisoma Waziri huyo hazioneshi picha kamili ya uhalisia wa uchumi wa Kenya na hivyo kuzipuuzilia mbali kuwa takwimu za kubuni tu.