Otuoma ashinda tikiti ya ODM Busia kwa kumbwaga Mutua

Muhtasari

• Otuoma alitangazwa mshindi Jumanne usiku na msimamizi wa uchaguzi Charles Tips baada ya kuzoa jumla ya kura 49,330 dhidi ya 30,696 za Mutua.

• Otuoma alimteua aliyekuwa mbunge wa Teso Kaskazini Arthur Odera mgombea mwenza wake.

• Otuoma atachuana na Lucas Meso wa Jubilee, Dan Mogoria wa DAP Kenya, na John Bunyasi wa  ANC.

Aliyekuwa Mbunge wa Funyula Paul Otuoma alipomchagua mgombea mwenza wake, mbunge wa zamani wa Teso Kaskazini Arthur Odera mnamo Aprili 5, 2022 katika Shule ya Sekondari ya Achiya Echakara iliyoko Teso Kaskazini. Picha: EMOJONG OSERE
Aliyekuwa Mbunge wa Funyula Paul Otuoma alipomchagua mgombea mwenza wake, mbunge wa zamani wa Teso Kaskazini Arthur Odera mnamo Aprili 5, 2022 katika Shule ya Sekondari ya Achiya Echakara iliyoko Teso Kaskazini. Picha: EMOJONG OSERE

Aliyekuwa mbunge wa Funyula Paul Otuoma atapeperusha bendera ya chama cha ODM katika kinyang'anyiro cha kumrithi Gavana Sospeter Ojaamong wakati wa uchaguzi wa Agosti 9.

Otuoma ambaye wakati mmoja alikuwa Waziri wa Michezo katika serikali ya Rais Mwai Kibaki alishinda uteuzi huo kwa kumbwaga mpinzani wake wa pekee, mwakilishi wa wanawake Florence Mutua.

Otuoma alitangazwa mshindi Jumanne usiku na msimamizi wa uchaguzi Charles Tips baada ya kuzoa jumla ya kura 49,330 dhidi ya 30,696 za Mutua.

Tangazo hilo lilitolewa katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Busia katika hafla iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Budalang’i Raphael Wanjala na mwenzake wa Funyula Wilberforce Mudenyo.

Otuoma sasa atachuana na Lucas Meso wa Jubilee, Dan Mogoria wa DAP Kenya, na Mbunge wa Nambale John Bunyasi ambaye anawania kiti hicho kwa tiketi ya  ANC IEBC itakapotangaza rasmi kuwa kampeni zimefunguliwa.

Naibu gavana Moses Mulomi alikuwa anatarajiwa kuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tiketi ya ODM lakini akajiondoa katika dakika za mwisho.

Otuoma alimteua aliyekuwa mbunge wa Teso Kaskazini Arthur Odera mgombea mwenza wake.

Otuoma baada ya ushindi wake alitoa wito kwa wanachama wa ODM katika kaunti hiyo kusalia na umoja na kuelekea kwa wa Agosti kama timu moja iliyoungana. Alisema huenda mifarakano ikavuruga chama kwani anaanza pia safari ya kumpigia kampeni kinara wa ODM Raila Odinga kwa safari yake ya ikulu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.  

"Tumefanya uchaguzi ambao ninaamini utaleta pamoja familia ya ODM kwa sababu tunapaswa kukumbuka huu ulikuwa mchezo kati ya wanachama wawili wa ODM," Otuoma alisema katika hotuba yake usiku wa kuamkia Jumanne. 

"Haya yalikuwa tu mashindano ya chama na litakuwa jukumu langu kuwaleta watu wote wa Busia pamoja ili tuweze kushinda wakati wa uchaguzi wa Agosti 9."Alisema vita makabiliano yaliyo mbele ya chama cha ODM katika kaunti hiyo bado ni mazito. 

"Baada ya haya ningetaka wanachama wote wa ODM wakutane ili tuelekeze macho yetu kwenye kinyang'anyiro cha Agosti 9 kwa sababu tunataka kuhakikisha kuwa chama chetu kinapata umaarufu zaidi kwa kuhakikisha kwamba tunawapigia kura wagombeaji wa ODM katika nyadhifa zote," alisema.  

“Lakini muhimu zaidi ni sisi kuhakikisha kuwa Raila Amollo Odinga anakuwa Rais wa tano. Najua Raila sasa amepokea wachezaji wazuri sana wa kisiasa na tutatekeleza wajibu wetu katika kuhakikisha kwamba tunapata kura nyingi iwezekanavyo kwa kiongozi wetu wa chama.” 

Katika kinyang'anyiro cha kupeperusha bendera ya nafasi ya mwakilishi wa wanawake, Catherine Omanyo alishinda mchujo huo baada ya kuwashinda wagombeaji wengine wanne. 

Omanyo, alipata kura 29, 273 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Beatrice Nakhooli aliyepata kura 17,641.Pamela Riziki Adhiambo aliibuka katika nafasi ya tatu kwa kura 16, 219 naye Cynthia Mutere akipata kura 8,691. 

Washindi wote walipokea vyeti vyao vya uteuzi wakati wa zoezi hilo ambalo lilikuwa na ulinzi mkali.