Toto: Kutana na mwanadada wa miaka 24 aliyeteuliwa wadhifa wa mwakilishi wanawake Bomet

Muhtasari

•Linet alipata shahada yake ya Bachelor of Business Administration hivi majuzi kutoka chuo kikuu cha Chuka.

•Allipata ushindi dhidi ya wanasiasa wengine wakiwemo Cecilia Mutai, Eunice Benson, Beatrice Tonui, Brenda Munai, Stacey Chepkemoi, Joan Towett, Susan Koech na Faith Chepkirui.

Linet 'Toto' Chepkorir atapeperusha bendera ya UDA katika kinyang'anyiro cha mwakilishi wanawake Bomet
Linet 'Toto' Chepkorir atapeperusha bendera ya UDA katika kinyang'anyiro cha mwakilishi wanawake Bomet
Image: HISANI

Linet Chepkorir almaarufu 'Toto' amekuwa gumzo mtandaoni katika kipindi cha masaa kadhaa ambacho kimepita baada yake kushinda tikiti ya UDA katika kinyang'anyiro cha mwakilishi wa wanawake Bomet.

Linet ambaye ana umri wa miaka 24 aliwashangaza wengi baada ya kuwabwaga miamba wa siasa Bomet na kunyakua tikiti ya UDA ambayo inashabikiwa sana  katika eneo hilo la bonde la ufa.

Machache tu yanajulikana kuhusu mwanasiasa huyo ambaye bila shaka ndiye mgombeaji mdogo zaidi kushinda kura ya mchujo katika Kaunti ya Bomet.

Linet alipata shahada yake ya Bachelor of Business Administration hivi majuzi kutoka chuo kikuu cha Chuka. Ni wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba.

Linet aliwahi kushtumiwa kwa kuingilia mkutano wa Ruto na viongozi wa bonde la ufa bila kibali na kuzuiwa kuingiwa.

Hata hivyo masaibu yake hayajamzuia kuwabwaga chini wanawake wengine 10 ambao walikuwa wanamezea mate tikiti ya UDA.

Linet allipata ushindi dhidi ya wanasiasa wengine wakiwemo Cecilia Mutai, Eunice Benson, Beatrice Tonui, Brenda Munai, Stacey Chepkemoi, Joan Towett, Susan Koech na Faith Chepkirui.