Asili ya kikabila haipaswi kutumika kama sababu ya kuchagua mgombea mwenza-Kalonzo

Muhtasari
  • Aliteta kuwa hata kama mienendo ingezingatiwa, yeye pia anatoka eneo la Mlima Kenya,

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka sasa anasema kwamba asili yake ya kikabila haipaswi kuwa jambo la kuzingatia wakati Azimio La Umoja One Kenya inamchagua mgombea mwenza.

Akizungumza katika ibada ya kanisa huko South C siku ya Jumapili, Kalonzo alielezea imani kuwa mienendo ya kikabila haitakuwa na jukumu katika kuchagua mgombea mwenza katika muungano huo.

Aliteta kuwa hata kama mienendo ingezingatiwa, yeye pia anatoka eneo la Mlima Kenya, akiwa amesoma Meru, na anazungumza Kimeru kwa ufasaha.

"Baadhi ya watu wanabishana kuwa mgombea mwenza lazima awe Mkikuyu. Mimi ninatoka mlimani. Nilisoma shule ya Meru ninazungumza kidogo Kimeru kwa hiyo ukweli mimi ni sehemu ya mlima," alisema Kalonzo.

"Hata kama unafanya ukabila katika nchi basi kumbuka pia jumuiya ya imani kwa kiasi kikubwa sana hawaamini migawanyiko ikiwa ni Wakamba, Wameru au Wakikuyu."

Aliendelea kusema kuwa atafanya mashauriano na kinara wa Azimio Raila Odinga na Rais Kenyatta ili kujadiliana kuhusu ni nani atakayechukua nafasi ya Bw Odinga.

"Tutashauriana na Raila na Uhuru kuhusu swali la mgombea mwenza, mimi niko katika chombo cha kufanya maamuzi. Kuna madaraja katika muundo wa uongozi wa muungano," alisema.

Haya yanajiri huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikizipa vyama vya kisiasa makataa ya kuwasilisha majina ya wagombeaji wao wa urais pamoja na wagombea wenza wao kufikia Aprili 28.