MC Jessy kuwania kiti cha ubunge wa Imenti Kusini kama Mgombea huru

Muhtasari
  • Naibu Rais William Ruto alisema mcheshi huyo atashiriki katika timu yake ya kampeni ya urais
MC Jessy na Naibu Rais William Ruto
Image: MC Jessy/INSTAGRAM

Mcheshi Jasper Muthomi, anayejulikana kama MC Jessy, ametangaza kuwa atawania kiti cha Mbunge wa Imenti Kusini katika uchaguzi wa Agosti 9 kama Mgombea Huru.

Kupitia akaunti yake rasmi ya Twitter mnamo Jumatatu, MC Jessy alitangaza kuwa bado yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuwawakilisha wakazi wa Imenti Kusini katika Bunge la Kitaifa.

"Imetumwa kama mshale kutoka kwa mkono wa shujaa. Tunaendelea….. Bado Tuko kwa mbio. Wacha tufanye hii Imenti Kusini, Agosti 9 ni," MC Jessy alisema.

Tangazo lake linakuja siku chache baada ya kutangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwa Mbunge wa Imenti Kusini Mwiti Kathaara.

Akitoa taarifa hiyo Jumatano, Naibu Rais William Ruto alisema mcheshi huyo atashiriki katika timu yake ya kampeni ya urais.

"MC Jessy (Jasper Muthomi) atajiunga na timu ya kampeni ya urais baada ya kuahirisha azma yake ya ubunge ili kumpendelea Mwiti Kathaara kuwania kiti cha Imenti Kusini," DP aliandika kwenye Twitter.

Mnamo Januari, mcheshi huyo alithibitisha kuwa amejiunga rasmi na chama kinachoongozwa na DP William Ruto, United Democratic Alliance, baada ya mashauriano mapana.