"Mt. Kenya ikimpa Raila mgombea mwenza, atapata 40% ya kura na Uhuru akimpigia kampeni atafika 55%" - Ngunjiri Wambugu

Muhtasari

• Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu ametoa tawimu zake jinsi Raila atapata asilimia 55 ya kura za Mt. Kenya.

Raila Odunga Akizungumza huko Baraka, Molo, kaunti ya Nakuru siku ya Jumatano Machi/2/2022
Image: Raila Odinga/TWITTER

Mbunge wa Nyeri Mjini Wambugu Ngunjiri amedokeza hesabu zake jinsi ambavyo kinara wa vuguvugu la Azimio la Umoja Raila Odinga atapata asilimia kubwa ya kura za Mlima Kenya na kumbwaga mpinzani wake wa karibu William Ruto ambaye anaonekana kupata ufuasi mkubwa kutoka eneo hilo lenye wapiga kura wengi zaidi.

Kupitia ukurasa wake wa facebook, Ngunjiri alidokeza hesabu zake akicheza na takwimu kwamba eneo hilo la Mlima Kenya kwa sasa lina wapiga kura waliojisajiri zaidi ya milioni 8.

Kulingana na Ngunjiri Wambugu, kinara wa ODM Raila Odinga kwa sasa ana uungwaji mkono wa 30% ambayo ni takribani kura milioni 2.4 za kura jumla milioni 8.

Alisema kwamba pindi tu vuguvugu la Azimio la Umoja watakapomtangaza mgombea mwenza kutokea eneo hilo, basi kura za Raila zitapanda na kufikia 40% ambayo ni sawia na kura milioni 3.6 za eneo hilo.

Mbunge huyo alizidi mbele na takwimu zake ambapo alisema kwamba pindi tu rais Uhuru Kenyatta atakapojibwaga uwanjani kumpigia kampeni Raila Odinga basi umaarufu wake utapanda hadi 55% ambayo ni sawa na kura milioni 4.4 za eneo la Mlima Kenya.

Hesabu hizi za Wambugu aidha zinazua maswali mengi ambapo baada ya kudokeza kwamba eneo hilo litapewa nafasi ya mgombea mwenza wa Raila ili asilimia iongezeke kutoka 30% hadi 40%.

Hili linamaanisha kwamba Kalonzo Musyoka ambaye pia anapigania nafasi hiyo huenda atarambishwa garasa la sivyo basi eneo la Mlima Kenya halitaongeza kuunga mkono Raila na kutimiza takwimu za Wambugu Ngunjiri.

Hapa kuna kivangaito kikali aisee!