UDA yatangaza marudio ya mchujo wa wabunge na wawakilishi wadi

Muhtasari
  • UDA yatangaza marudio ya mchujo wa wabunge na wawakilishi wadi
UDA yadai uchunguzi juu ya machafuko yaliyoharibu mkutano wa DP Ruto Jacaranda
Image: Mercy Mumo

Chama cha United Democratic Alliance kinatazamiwa kufanya marudio na mazoezi mapya ya uteuzi Jumatano na Alhamisi wiki hii.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi Anthony Mwaura katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili jioni alisema kura ya mchujo iliyoratibiwa itafanywa kwa kufuata kikamilifu kanuni za chama.

Eneo bunge la Mogotio katika kaunti ya Baringo litafanya uchaguzi wa marudio kufuatia maandamano ya baadhi ya wagombea kwamba zoezi hilo halikuwa la uwazi.

Mwaniaji Reuben Kiborek alipinga kutunukiwa tikiti kwa mbunge aliye madarakani Daniel Kamuren ambaye alitangazwa mshindi wa zoezi hilo lililofanyika Alhamisi.

Zoezi hilo litarudiwa Alhamisi, Aprili 21.

Majimbo ya Kamukunji na Roysambu jijini Nairobi yatafanya marudio ya uteuzi Jumatano, Aprili 20.

Chama kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto pia kitaendesha mchujo mpya wa viti vya wabunge.

Chama hicho kitakuwa na uteuzi Embakasi Mashariki siku ya Jumatano. Majimbo ya Kilome na Makueni yataandaa lao siku ya Alhamisi.

Katika maeneo bunge ya Mathare na Dagoretti Kaskazini, chama cha UDA kitaendesha uteuzi wa pamoja na chama cha ANC Jumatano ili kubainisha wagombeaji hodari ambao watawania tiketi ya Kenya Kwanza Alliance.

Chama cha UDA pia kimepanga marudio ya mchujo wa Wabunge wa Mabunge ya Kaunti katika wadi kadhaa za Nairobi siku ya Jumatano. Wadi hizo ni pamoja na Landi Mawe, Jiji la Nairobi Kati, Ngara, Pangani na Ziwani/Kariokor katika eneo bunge la Starehe.

Katika eneo bunge la Embakasi Kaskazini, kura za marudio zitafanywa katika wadi za Dandora (ii), Dandora (iii) na Dandora (iv).

Katika eneo bunge la Embakasi Magharibi, chama cha UDA kitaendesha kura za marudio katika wadi ya Mowlem pekee.

Wadi za Roysambu, Githurai, Kahawa na Kahawa magharibi huko Roysambu pia zitakuwa na marudio ya mchujo.

Katika eneo bunge la Kamukunji, kura zitarudiwa katika wadi za Airbase, California, Eastleigh Kaskazini, Eastleigh Kusini na Pumwani.