"Uwezo wangu wa kiakili uko juu kuliko wako!" Babu Owino amwambia Nelson Havi

Muhtasari

• Mbunge Babu Owino amepakia cheti chake na cha Nelson Havi akimtaka mwanasheria huyo kulinganisha vizuri aone kama anamshinda.

• Owino amemtaka Havi kumheshimu kwa vile hawezi kumfikia katika masomo ya sheria.

Babu Owino
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amewaacha wengi vinywa wazi baada ya kupakia kwenye ukurasa wake wa Facebook stakabadhi zinazoonekana kama vyeti vya matokeo viwili ambavyo alikuwa akilinganisha matokeo yake na yale ya wakili mwanasheria na ambaye anawania ubunge Westlands, Nelson Havi enzi zao wakiwa shule za upili.

Katika stakabadhi hizo ambazo haijulikani Owino alipata wapi ya Havi anajidai kwamba matokeo yanaonesha yeye ni msomi zaidi kuliko wakili Havi ambaye alikuwa rais wa wanasheria nchini LSK.

Hii si mara ya kwanza ambapo wawili hao wanaendeleza vita vya ubabe huku wakati mmoja Havi akimkashfu Owino kwa vitendo vyake ambapo alisema kwamba mbunge huyo ambaye pia anashahada ya sheria kutoka chuo cha Nairoi, tawi la uanasheria la Parklands anadhalilisha chuo hicho kwa vitendo vyake.

Babu Owino wakati huo alimjia juu Havi kwa kumzomea kwamba yeye kando cha kuchaguliwa kuwa rais wa wanasheria LSK, hana lolote na kusema kwamba anamshinda pakubwa katika ujuzi wa sheria.

Ni kama safari hii Owino amekuja na Ushahidi wa kutetea matamshi yake kwamba anamshinda Havi katika uanasheria ambapo ameamua kulinganisha jinsi ambavyo walikuwa wakifanya katika masomo ya shule za upili.

“Linganisha na utofautishe Nelson Havi na ujue kwamba uwezo wangu wa kiakili uko juu zaidi yako. Acha kukimbiza usichoweza kukamata. PASS katika LLB LAW. Nzi anaweza kumsumbua simba kuliko vile simba anavyoweza kumsumbua nzi,” aliandika Babu Owino kwa kile kilionekana kama anamzomea Nelson Havi.

Babu Owino analenga kukitetea kiti chake cha ubunge Embakasi Mashariki kupitia tiketi ya ODM huku Nelson Havi akilenga kuwa mbunge wa Westlands kwa tiketi ya UDA kumrithi Tim Wanyonyi anayelenga ugavana Nairobi kwa tiketi ya ODM