Huenda SRC ikapunguza mishahara ya wabunge kuiana na viwango vya elimu - Muturi

Muhtasari

• Maseneta pia waliunga mkono mswada unaofutilia mbali hitaji la digrii kwa wanaowania ubunge na MCA. 

• "Iwapo mishahara yao itapunguzwa watajilaumu wenyewe kwa sababu wao ndio wanaopendekeza kushusha viwango vya hitaji la kisomo,” Muturi alisema. 

Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Image: WILFRED NYANGARESI

Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi amewasuta wabunge kuhusu kupunguzwa kwa viwango vya masomo vinavyohitajika kwa mtu kuwa mbunge. 

Akizungumza wakati wa mahojiano katika runinga ya NTV siku ya Jumatatu, Muturi alisema wabunge hao ndio wa kulaumiwa iwapo Tume ya Mishahara na Marupurupu itaamua kupunguza mishahara yao. 

Wabunge walikuwa wametetea kupunguzwa kwa viwango vya hadhi ya masomo hadi tu cheti cha sekondari kwa wanaotaka Ubunge. 

Maseneta pia waliunga mkono mswada unaofutilia mbali hitaji la digrii kwa wanaowania ubunge na MCA. 

“Iwapo mishahara yao itapunguzwa watajilaumu wenyewe kwa sababu wao ndio wanaopendekeza kushusha viwango vya hitaji la kisomo,” Muturi alisema. 

"Ikiwa unataka watu ambao hawawezi kusoma yaliyomo katika makadirio ya bajeti waende Bungeni basi SRC iko huru kusema 'ikiwa hawawezi kusoma yaliyomo kwenye bajeti, kwa nini tuwalipe kiasi hicho?' SRC itakuwa haki." 

Muturi aliendelea kusema kuwa..."Ikiwa utaweka alama ya chini sana, basi usilalamike ni kiwango kipi cha mishahara ambayo SRC itapendekeza kwa wabunge,". 

Wiki jana, Mahakama ya Juu iliamua kwamba wanaotaka kuwa wabunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 hawahitaji digrii za chuo kikuu. Jaji Anthony Mrima alisema kuwa Kifungu cha 22(1)(b) (i) cha Sheria ya Uchaguzi kinachotaka wabunge kuwa na digrii ni kinyume cha Katiba.